Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Thursday 9 January 2014

SIMBA SC NA AZAM KATIKA BONGE LA MTIHANI KOMBE LA MAPINDUZI LEO

Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
TIMU mbili maarufu za Uganda, URA na KCC, leo zinaingia vitani dhidi ya timu nyingine mbili kubwa Tanzania, Azam FC na Simba SC za Dar es Salaam katika Nusu Fainali za Kombe la Mapinduzi, Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Timu ya Halmashauri ya Jiji la Kampala (KCC) itaanza kumenyana na Azam FC Saa 10:00 jioni kabla ya timu ya Mamlaka ya Mapato Uganda (URA) kuumana na Simba SC Saa 2:00 usiku.
Ni mtihani mgumu kwa Tanzania na kuna hatari Fainali ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu ikakutanisha timu ya nyumbani na ya Uganda, au zote za wageni kutokana na ukweli kwamba KCC na URA ni tishio.

Kikosi cha Simba SC Kombe la Mapinduzi


Mabingwa watetezi Azam FC Kombe la Mapinduzi
Timu zote zina safu kali za ushambuliaji na hilo linadhihirishwa na idadi ya mabao waliyovuna hadi sasa kwenye mashindano hayo, kuwa mengi kuliko ya timu nyingine na pia wachezaji wake ndio wanaongoza kufunga hadi kwenye sasa michuano hii.
Owen Kasuule wa URA ana mabao manne, wakati mchezaji mwenzake wa timu hiyo, Feni Ali ana mabao matatu na Herman Waswa wa KCC ana mabao mawili sawa na Ramadhani Singano na Amri Kiemba wa Simba SC, Brian Umony wa Azam FC na Mwinyi Mngwali wa Chuoni.
Makipa Mwadini Ali wa Azam na Ivo Mapunda wa Simba ni tumaini kubwa la matokeo mazuri kwa timu za Tanzania leo, kutokana na umahiri wao uliofanya hadi kufika hatua hii wawe hawajafungwa hata bao moja.
Kwa ujumla Azam FC na Simba SC zimeonyesha kuwa na safu imara za ulinzi na kuwa na mwanzo mzuri chini ya makocha wapya, Mcroatia Zdravko Logarusic wa Wekundu wa Msimbazi na Mcameroon, Joseph Marius Omog wa timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa.
Lakini hata safu za kiungo na ushambuliaji za timu hizo zinaridhisha kwa sasa, Simba ikiwa na wakali kama Jonas Mkude, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ na Amri Kiemba katikati na mbele Amisi Tambwe na Ramadhani Singano ‘Messi’, wakati Azam ina Himid Mao, Kipre Balou na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ katikati na Brian Umony na Kipre Tchethe mbele.
Timu hizo za Dar es Salaam zilianza mashindano haya taratibu na kadiri yanavyosonga mbele zimekuwa zikiimarika zaidi kama zilivyoonekana juzi katika hatua ya Robo Fainali.
Azam iliifunga 2-0 Cloves Uwanja wa Gombani Pemba juzi mchana, sawa na Simba SC ilivyoifunga Chuoni Uwanja wa Amaan usiku.
Kutakuwa na mapumziko ya siku mbili baada ya mechi za leo na Fainali ya michuano hiyo itachezwa Jumatatu Saa 10: 00 jioni na hakutakuwa na mechi ya mshindi tatu. Kila la heri Simba SC na Azam FC Kombe la Mapinduzi 2014.

No comments:

Post a Comment