Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Friday, 4 April 2014

HALI YA SHUMACHER YAIMARIKA


Bingwa wa zamani wa mbio za magari ya langalanga ya F1, Michael Schumacher ameanza kuonyesha hali ya kupata fahamu baada ya miezi kadha ya kuwa katika hali ya kutojitambua.

Wakala wake Sabine Kehm amesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amesema Schumacher "anaendelea vizuri", akisema kwamba wana "uhakika"wa kupona kwake.

Madaktari nchini Ufaransa wanafanya jitihada za kumwondoa katika hali ya kutojitambua, bingwa huyo mara saba wa F1

CANNAVARO AINGIA KAMBINI YANGA SC TAYARI KWA MECHI NA JKT RUVU JUMAPILI

Na Renatus Mahima, Dar es Salaam
NAHODHA wa Yanga SC, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ jana ameingia kambini katika hoteli ya Kiromo, Bagamoyo, Pwani kujiunga na wenzake kwa ajili ya mchezo wa Jumapili dhidi ya JKT Ruvu.
Cannavaro alikuwa anaumwa Malaria tangu arejee kutoka Tanga mapema wiki hii, ambako mwishoni mwa wiki timu yake ilifungwa mabao 2-1 na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani.
Mganda, Emmanuel Okwi bado hajapatikana na viongozi wanalalamika hata simu yake haipatikani, wakati mgonjwa mwingine wa Malaria, kiungo Haruna Niyonzima naye bado anajiuguza nyumbani kwake.

Kapteni kambini; Nadir Haroub 'Cannavaro' ameingia kambini jana, lakini Okwi bado hapatikani

Beki Kevin Yondan ameondolewa katika programu ya mchezo ujao kwa kuwa anatumikia adhabu ya kadi mbili za njano na hayupo kambini na mchezaji mwingine ambaye sababu za kutokuwepo kwake kambini hazijulikani ni Athumani Iddi ‘Chuji’, ingawa watu wake wa karibu wanasema ana matatizo ya kifamilia.
Habari njema tu ni kwamba, makipa wote watatu waliosajiliwa msimu huu Yanga SC, Juma Kaseja, Deo Munishi ‘Dida’ na Ally Mustafa ‘Barthez’ wapo kambini na wanaendelea na mazoezi.
Baada ya kupoteza pointi tatu zinazowafanya waachwe mbali na kidogo na Azam FC katika mbio za ubingwa, Yanga SC itashuka dimbani Jumapili hii kumenyana na timu nyingine ya Jeshi la Kujenga Taifa, JKT Ruvu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Azam FC inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 53 baada ya kucheza mechi 23, ikifuatiwa na Yanga SC yenye pointi 46 za mechi 22 na Mbeya City yenye pointi 45 za mechi 23 ni ya tatu.
Wakati Yanga SC itacheza na JKT Ruvu Jumapili Uwanja wa Taifa, Mbeya City itacheza na Ashanti United Jumamosi Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Azam FC ilikuwa icheze na Ruvu Shooting Jumapili hii pia, Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani lakini mchezo huo umesogezwa mbele hadi Aprili 9, kutokana na timu hiyo kuwa na wachezaji wengi katika kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes.
Ngorongoro Heroes ipo Nairobi, Kenya tangu jana kwa ajili ya mechi ya kuwania kucheza Fainali za Vijana Afrika, itakayochezwa Jumapili ya Aprili 6 mwaka huu Uwanja wa Machakos ulioko kilometa 80 kutoka jijini Nairobi na Azam ina wachezaji zaidi ya watano kwenye kikosi hicho.
Hao ni Aishi Manula, Bryson Raphael, Gardiel Michael, Kevin Friday, Mudathir Yahya, Farid Mussa na Hamad Juma.

Monday, 31 March 2014

WAHABESHI WAMZUIA KOCHA MPYA STARS KUJA DAR

Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
KOCHA mpya wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mholanzi Martinus Ignatius ‘Mart’ Nooij sasa atawasili mwishoni mwa mwezi huu badala ya leo kama ilivyotarajiwa, imefahamika.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi aliahirisha Mkutano na Waandishi wa Habari uliokuwa ufanyike Machi 24 mwaka huu kumtaja rasmi mwalimu huyo, ili zoezi hilo lifanyike atakapowasili- na sasa atalazimika kusubiri hadi kuanzia Aprili 20.

Kocha ambaye wa Stars Mart Nooij aliyekuwa awasili leo, sasa anatarajiwa kutua nchini kuanzia Aprili 20, mwaka huu

Hiyo inafuatia klabu yake, St George ya Ethiopia kumbana asiondoke hadi itakapopata mwalimu mpya, zoezi ambalo Nooij anaisaidia timu hiyo kuhakikisha inapata kocha mwingine bora.
BIN ZUBEIRY inafahamu tayari Nooij amekwishasaini Mkataba wa miaka miwili na TFF- ingawa sasa ujio wake unakumbwa na mizengwe.
Ulikuwa mchakato makini, uliohusisha wataalamu na washauri wa kimataifa juu ya masuala ya ufundi ya soka ambao umefanikisha kupatikana mwalimu huyo wa Kiholanzi aliyezaliwa Julai 3, mwaka 1954 mjini Beverwijk, Uholanzi.
Nooij amewahi kuwa mwalimu maalum katika programu za maendeleo ya soka katika Chama cha Soka Uholanzi (DFA) na pia amewahi kufundisha timu ya EVC 1913 ya Marekani na baadaye Kazakhstan.
Alikuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Burkina Faso katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2003 na mwaka 2004 alikuwa kocha wa muda wa klabu ya FC Volendam ya Uholanzi.
Mwaka 2007 aliteuliwa kuwa kocha wa Msumbiji na akaiwezesha kufuzu kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2010, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza Mambas wanashiriki AFCON baada ya msoto wa miaka 12.
Hata hivyo, katika fainali hizo, Msumbiji ilishika mkia katika kundi lake baada ya kuambulia sare moja na kufungwa mechi mbili. Baada ya kukosa tiketi ya AFCON 2012, Nooij akajiuzulu Septemba mwaka 2011 na nafasi yake kuchukuliwa na Mjerumani, Gert Engels.
Aprili 19 mwaka 2012, aliajiriwa na klabu ya Santos ya Afrika Kusini, ambako hata hivyo alifukuzwa Desemba 18, mwaka 2012 na kunyakuliwa na St George ya Ethiopia anakoendelea na kazi hadi sasa.
Baada ya kusaini Mkataba wa miaka miwili na TFF kuja kuifundisha Stars, Nooij anasubiri barua maalum ya kuruhusiwa kuondoka baada ya kukamilisha taratibu za kuvunja Mkataba uliokuwa unaelekea ukingoni na klabu hiyo ya Addis Ababa.

TIMU YA OKWI, ETOILE YAPETA AFRIKA

ETOILE du Sahel ya Tunisia imeitoa SuperSport United ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 5-1 katika Kombe la Shirikisho Afrika baada ya juzi kuilaza mabao 4-1 Afrika Kusini.
Timu hiyo ya zamani ya mshambuliaji wa Yanga SC, Emmanuel Okwi katika mchezo wa kwanza ilishinda bao 1-0 na sasa inakwenda Hatua ya 16 Bora ambako itamenyana na moja ya timu zilizotolewa katika Ligi ya Mabingwa kupata tiketi ya kucheza Hatua ya Makundi.


Katika mechi nyingine za juzi, Bayelsa United ya Nigeria iliitoa How Mine ya Zumbabwe kwa jumla ya mabao 3-2, ikianza kufungwa 2-1 ugenini na Jumamosi kushinda 2-0 nyumbani, Difaa El Jadida ya Morocco imeitoa AS Kigali kwa jumla ya mabao 3-1 ikishinda 3-0 juzi baada ya kufungwa 1-0 katika mchezo wa kwanza.
Katika mechi za jana, ASEC Mimosas ya Ivory Coast iliifumua CS Constantine ya Algeria mabao 6-0, Petro Atletico ya Angola iliifunga 1-0 Ismailia ya Misri baada ya sare 0-0 katika mchezo wa kwanza.
Djoliba ya Mali ilisonga mbele kwa ushindi wa penalti 3-2 baada ya sare ya jumla ya 2-2 na Wadi Degla ya Misri kila timu ikishinda 2-0 nyumbani kwake, CA Bizertin ya Tunisia iliifunga 2-1 Warri Wolves ya Nigeria baada ya sare ya 0-0 katika mchezo wa kwanza na Zesco United ya Zambia imeifunga 1-0 Medeama ya Ghana baada ya kufungwa 2-0 katika mchezo wa kwanza, hivyo imeaga.

ERITREA YAJITOA AFCON 2015

SHIRIKISHO la Soka Eritrea limelitaarifu Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kujitoa kwenye michuano ya 30 ya Kombe la Mataifa ya Afrika ambayo fainali zake zitafanyika nchini Morocco mwaka 2015.
Taarifa ya CAF iliyotumwa BIN ZUBEIRY, imesema kwamba kwa maana hiyo, mchezo wa hatua ya mchujo baina ya Eritrea na Sudan Kusini umefutwa na sasa wapinzani wao hao wanafuzu moja kwa moja hatua inayofuata.