Na Salum Esry, Alexandria
YANGA SC imetolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya jumla ya kufungana bao 1-1 na Al Ahly katika mechi mbili za Dar es Salaam na Alexandria.
Yanga SC iliyoshinda 1-0 wiki iliyopita Dar es Salaam, leo imefungwa 1-0 baada ya dakika 90 kwenye mchezo wa marudiano Uwanja wa Border Guard mjini Alexandria.
Kipa Deo Munishi ‘Dida’ alipangua penalti mbili mfululizo ya nne na ya tano zilizopigwa na Saed Mowaeb na Hossan Ashour, wakati za Abdalllah Said, Gedo, Mahmoud Trezeguet na Mohamed Nagieb zilimpita, lakini Yanga SC nao wakakosa penalti mbili mfululizo ya nne na ya tano.

Yanga na Al Ahly wakimenyana leo Cairo
Oscar Joshua alipiga penalti nzuri ikaguswa na kipa Sherif Ekramy Ahmed na kugonga mwamba na kurudi uwanjani, wakati Said Bahanuzi akapiga nje upande wa kushoto wa lango.
Sherif Ekramy Ahmed alipangua penalti ya mwisho ya Yanga SC iliyopigwa na Mbuyu Twite na kuwavusha Hatua ya 16 Bora mabingwa hao wa Afrika.
Waliofunga penalti za Yanga SC ni Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Didier Kavumbangu na Emmanuel Okwi.
Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao, Yanga SC wakicheza mchezo wa kujihami na mashambulizi ya kushitukiza.
Mrisho Ngassa alicheza vyema katika safu ya kiungo mchezeshaji akiwapa pasi nzuri washambuliaji Emmanuel Okwi, Simon Msuva, Didier Kavumbangu na Hamisi Kiiza.
Kiungo mkabaji Frank Domayo alishirikiana vizuri na mabeki wa kati Kevin Yondan na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wakati mabeki wa pembeni Mbuyu Twite kulia na Oscar Joshua kushoto walifanya kazi nzuri ya kuzuia na kusaidia mashambulizi.