Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Saturday, 15 March 2014

YANGA SC HAIJASHINDA MECHI MOROGORO MBELE YA MTIBWA SUGAR KWA MIAKA MITANO SASA, LEO ITAVUNJA MWIKO?

Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
YANGA SC haijashinda mechi Uwanja wa Jamhuri Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar kwa miaka minne sasa na leo inashuka kwenye Uwanja huo kumenyana na Wakata Miwa hao wa Manungu.
Septemba 19 mwaka 2009 ndipo Yanga SC iliposhinda kwa mara ya mwisho Uwanja wa Jamhuri wakati huo ikiwa chini ya kocha Mserbia, Profesa Dusan Savo Kondic na tangu hapo kila inapokwenda huko matokeo mazuri kwao yamekuwa sare.
Wachezaji wa mwisho kuipa Yanga SC ushindi Uwanja wa Jamhuri dhidi ya Mtibwa walikuwa ni Nurdin Bakari aliyefunga dakika ya 55 na Mrisho Ngassa dakika ya 57, lakini zaidi ya hapo mechi zilizofuata Wana Jangwani hao ama wamefungwa, au kutoa sare.
Watavunja mwiko? Kikosi cha sasa cha Yanga SC kinakabiliwa na changamoto ya kuvunja mwiko wa kutoshinda mechi Uwanja wa Jamhuri mbele ya Mtibwa Sugar kwa miaka mitano sasaNa wote leo hawatakuwepo Uwanja wa Jamhuri, Nurdin aliachwa msimu uliopita akaenda Rhino Rangers ya Tabora, wakati Mrisho Ngassa ataukosa mchezo wa leo kutokana na kuwa majeruhi.
Haijalishi- kama anakosekana Ngassa lakini kikosini kuna wakali wengine wanaoifanya Yanga SC iitwe timu tishio zaidi katika Ligi Kuu ya Bara kama Emmanuel Okwi, Hamisi Kiiza wote kutoka Uganda, Didier Kavumbangu wa Burundi, Haruna Niyonzima wa Rwanda na wazalendo kama Simon Msuva katika safu ya ushambuliaji.
Ngassa amekuwa chachu ya ushindi katika mechi zilizopita za Yanga SC na leo anakosekana kwa mara ya kwanza katika mchezo muhimu, maana yake macho ya mashabiki wa timu hiyo yatakuwa kwa akina Okwi, Kiiza, Kavumbangu na Msuva.
Makocha waliotangulia Mserbia Kosta Papic, Mganda Sam Timbe, Mbelgiji Tom Saintfiet na Mholanzi Ernie Brandts hawakuwahi kushinda Morogoro dhidi ya Mtibwa na wote walikuwa wanasema sababu za kupata wakati mgumu Uwanja wa Jamhuri ni ubovu wa eneo la kuchezea.
Kocha mpya wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm amecheza mechi moja tu ugenini dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ambako alitoa sare na akalalamikia hali ya Uwanja.
Pluijm ambaye inaaminika ameibadili Yanga SC na sasa inacheza vizuri, leo anaingiza timu kwenye Uwanja mwingine ambao umekuwa ukilalamikiwa kwa ubovu wa eneo la kuchezea na mbaya zaidi atamkosa Mrisho Ngassa.
Okwi tangu akiwa Simba SC alikuwa hawezi kuwika nje ya Uwanja wa Taifa katika Ligi Kuu, angalau Kiiza amekuwa akifunga kwenye viwanja vibaya kama Mkwakwani na Kaitaba.
Hussein Javu aliyekuwa anainyanyasa Yanga SC akiwa na jezi ya Mtibwa Sugar miaka ya karibuni, msimu huu amesajiliwa na Wana Jangwani hao ingawa hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza.




+6
Mshindi wa mwisho: Mrisho Ngassa aliifungia Yanga SC bao la ushindi ikishinda mara ya mwisho dhidi ya Mtibwa Sugar Morogoro Septemba 19, mwaka 2009, lakini leo ataukosa mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi

Lakini Mtibwa imeziba pengo la Javu kwa kumsajili mshambuliaji mwingine mzuri, Abdallaha Juma na bado ina wakali wengine kama Juma Luizio, Jamal Mnyate na Shaaban Kisiga ‘Malone’.
Kwa kawaida Mtibwa hata iwe haina makali, unapowadia mchezo dhidi ya Yanga SC huwa inabadilika mno- hivyo kufungwa nyumbani hadi na Prisons haimaanishi kama watakuwa wepesi leo Jamhuri.
Mechi nyingine za ligi hiyo leo ni kati ya wenyeji, Azam wanaoikaribisha Coastal Union ya Tanga Uwanja wa Azam Complex. Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, wakati Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera Sugar watakuwa wenyeji Prisons ya Mbeya.
Hadi sasa, mbio za ubingwa wa Ligi Kuu zinaonekana kuwa za Yanga na Azam FC, ingawa bado huwezi kuziondoa moja kwa moja Mbeya City na Simba SC kulingana na pointi zao na idadi ya mechi walizobakiza- kwani iwapo vinara hao watapoteza mwelekeo, mambo yanaweza kugeuka.
Azam FC ipo kileleni kwa pointi zake 40 baada ya kucheza mechi 18, ikifuatiwa na Mbeya City yenye pointi 39 baada ya kucheza mechi 21, wakati Yanga SC yenye pointi 38 baada ya mechi 17 ni ya tatu na Simba ipo nafasi ya nne kwa pointi zake 36 baada ya mechi 21.
REKODI YA YANGA SC NA MTIBWA TANGU 2009

Septemba 19, 2009; Mtibwa Sugar 1-2 Yanga SC
Septemba 15, 2010; Mtibwa Sugar 1-1 Yanga SC
Februari 2, 2011 Yanga SC 0-1 Mtibwa Sugar
Septemba 7, 2011 Mtibwa Sugar 0-0 Yanga SC
Februari 8, 2012 Yanga SC 3-1 Mtibwa Sugar
Septemba 19, 2012 Mtibwa Sugar 3-0 Yanga SC
Februari 2, 2013 Yanga SC 1-1 Mtibwa Sugar
Oktoba 6, 2013 Yanga SC 2-0 Mtibwa Sugar
(Zilizokolezwa wino mweusi ni mechi zilizochezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro)

No comments:

Post a Comment