Soka na siasa kwa upande mwingine vyote vina vitu kadhaa vyenye ufanano kuliko ambavyo wengi wangeweza kudhania.
KWA hapa England watu wanapozungumzia siasa hujenga taswira ya wanaume na wanawake, wengi wao wazee wakiwa wamekaa kwenye mabenchi ya kijani bungeni.
Watu hao huwa kwenye ukumbi wa kawaida, tofauti kabisa na ule wa kisasa mno wa Dodoma nyumbani Tanzania.
Siasa ya hapa inachukuliwa na wengi kuwa ni masuala yanayochosha, yasiyo na mvuto yanayohusisha mijadala mingi bila kufikia hitimisho la pamoja.
Unapozungumzia soka kwa upande mwingine, picha inayowajia wengi ni ya wachezaji nyota wenye mvuto na viwango vya hali ya juu kisoka katika Ligi Kuu England, maarufu EPL. Naam, wanafikiria pia nje ya uwanja jinsi wachezaji hao, baadhi wakiwa ni mamilionea vijana, wakiendesha magari ya kisasa na ya bei mbaya mitaani, wakiishi maeneo ya hali ya juu ambayo watu wengi hawana hata ndoto za kuishi huko.