Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Friday, 20 September 2013

MAKALA;Soka na siasa katika uhusiano wa kipekee-1




Soka na siasa kwa upande mwingine vyote vina vitu kadhaa vyenye ufanano kuliko ambavyo wengi wangeweza kudhania.
KWA hapa England watu wanapozungumzia siasa hujenga taswira ya wanaume na wanawake, wengi wao wazee wakiwa wamekaa kwenye mabenchi ya kijani bungeni.


Watu hao huwa kwenye ukumbi wa kawaida, tofauti kabisa na ule wa kisasa mno wa Dodoma nyumbani Tanzania.


Siasa ya hapa inachukuliwa na wengi kuwa ni masuala yanayochosha, yasiyo na mvuto yanayohusisha mijadala mingi bila kufikia hitimisho la pamoja.


Unapozungumzia soka kwa upande mwingine, picha inayowajia wengi ni ya wachezaji nyota wenye mvuto na viwango vya hali ya juu kisoka katika Ligi Kuu England, maarufu EPL. Naam, wanafikiria pia nje ya uwanja jinsi wachezaji hao, baadhi wakiwa ni mamilionea vijana, wakiendesha magari ya kisasa na ya bei mbaya mitaani, wakiishi maeneo ya hali ya juu ambayo watu wengi hawana hata ndoto za kuishi huko.www.hakleo.blogspot.com


Watu walio katika makundi mawili hayo wapo mbalimbali, lakini ukweli ni kwamba wakati wote soka na siasa zina uhusiano wa kipekee.


Soka na siasa kwa upande mwingine vyote vina vitu kadhaa vyenye ufanano kuliko ambavyo wengi wangeweza kudhania.


Makundi yote mawili hutazamwa na mamilioni ya watu kwa njia mbalimbali, huwa asili ya mfarakano na ubaguzi.


Kwa namna tofauti wote hujawa matumaini makubwa, hujimwaga kwenye sherehe au hafla kubwa kubwa za kula, kunywa na kucheza.


Wote wawili pia kuna wakati hujikuta katika shangwe, nderemo na vifijo vya ushindi mkubwa wakati adui ameanguka, au huwa katika kilio wanaposhindwa.


Kama ilivyo kwa makundi yote, kuna kutokuelewana na kupambana ndani kwa ndani wakati wa safari za kufikia malengo yaliyowekwa awali.


Ni kawaida kwenye maeneo yote mawili yaani soka na siasa kukuta washiriki wake wakilipuka kwa hasira kubwa na kushindwa kujizuia nyakati fulani na pia kuna utaratibu wa hatua za kinidhamu dhidi ya watovu wa nidhamu.


Baadhi ya wachezaji huweza kuchokwa mapema katika timu na kufikia hatua ya kupigwa bei haraka wakati wengine hubakia sehemu moja (iwe chama au klabu) kwa muda mrefu kupindukia.


Kwa pande zote mbili, kuna wale wanaotajwa kuwa mfano, kivutio na kichocheo kwa jamii na vijana na wakatangazwa kote duniani.


Hao huanza kuhusishwa na watu maarufu kimataifa, iwe ndani ya taifa hili au hata kwingineko duniani, hivyo wadau huanza kuimba sifa zao kama mashujaa wao.


Wapo ambao huwa na ushirikiano mkubwa sana na wenzao kwenye kundi, wachache huibuka kuwa viongozi wazuri wa kuwapangia wenzao njia nzuri, lakini kuna ambao huibuka kwa vipindi na kujiamulia wenyewe ya kufanya bila kujali kanuni walizowekewa.


Vyote viwili, soka na siasa hufuatiliwa kwa karibu na wadau wengi, vyombo tofauti vya habari huwachimba vilivyo ikiwamo mambo yao ya faragha.


Naam, wanasiasa na wanasoka hufuatwa kwa karibu, hasa wanapoanza uhusiano wa kimapenzi, uwe wa kifamilia au wa nyumba ndogo, lakini hufika mahali wakalipuliwa na kusababisha mwangwi mkubwa mbele ya jamii.


Wafuasi au mashabiki wao huwa hawaambiliki, wakishawapenda huwafuata kama kumbikumbi na wakifika mahali wakawachoka huweza kubadilika kabisa kama kinyonga na kuwaadhibu kwa njia mbalimbali.


Katika nyakati kadhaa, wanasiasa au wanasoka huwa na uwezo wa kuunganisha taifa, nyakati muhimu wanapoonyesha heshima na wenyewe kuheshimiwa au nyakati za ajali, msiba na pia nyakati zile za furaha kama ushindi mkubwa unapopatikana. Kwa chama kama cha Labour hapa Uingereza, soka ni njia inayoweza kutumiwa kukabiliana na masuala makubwa kwenye majimbo mbalimbali nchini ikiwamo kukosekana matumaini.


Hii ni kwa sababu soka haina mipaka; haijali hadhi ya mtu, asili, rangi wala dini. Haina athari katika uwezo wa mchezaji kung’ara katika dakika 90 za mechi kwenye viwanja vya kijani kabisa kote England, rangi iliyo sawa na mabenchi niliyosema awali kule bungeni Westminster.


Kwa upande mwingine hutoa taswira ya masuala mengine mengi ya jamii kama wanawake kulipwa kidogo kuliko wenzao wanaume, ngono na starehe za kupitiliza, ubaguzi wa rangi tena katika hali mbaya, upinzani kwa masuala ya ushoga, migongano juu ya haki za Waislamu na Wayahudi. Yote hayo pamoja na ubaya wake, huvuta hisia za wengi na kurushwa na vyombo vya habari kutokana na uzuri wa mchezo huu wa soka na jinsi unavyopendwa.


Mvuto na athari zake kwa watu wa familia za kawaida ni kubwa sana. Laiti kama si soka, basi jamaa zangu akina Steven Gerrard na Wayne Rooney wangekuwa wakihangaika kugonga vyuma kwenye magereji kule Liverpool ili kupata chakula cha watoto.


Leo si hivyo, wanatamba kwa mishahara ya mamilioni, majumba ya kifahari na magari ya anasa yaendayo kasi, wakizuga na vimwana wao mitaani.









Ndivyo ingekuwa pia kwa wanasoka wengine mahiri wala hapangekuwa na stori kubwa zinazouza magazeti na kuvuta matangazo ya mabilioni ya pauni kila mwaka.


Ndio ukweli maana leo hii Mesut Ozil wa Arsenal labda angekuwa akihenya kwenye mashamba ya mkonge au chai, Robin van Persie akiuza kahawa hotelini Uholanzi na Arsene Wenger akifundisha uchumi aliosomea chuo kikuu.


Pengine John Terry angekuwa fundi cherehani na Frank Lampard akisimamia biashara za baba yake au akikatisha tiketi za treni hapo kwenye kituo kikubwa cha Paddington, Mario Balotelli akiwa mchimba mawe au mfyatua matofali huku Ryan Giggs akiwa dereva wa malori makubwa.


Lakini si hivyo, soka imekuja na makubwa yake, ina uwezo mkubwa wa kubadili maisha na imefanya hivyo na kuwa tofauti mno na kazi nyingine, maana nani analipwa zaidi ya nyota wakubwa wa soka?


Michezo mingine imefurukuta lakini haifikii soka na kwa msingi huu ndio maana nasema kwamba siasa inaweza kujifunza kwenye soka.


Wakati wenzangu wanapojitahidi kujenga Bunge wanalotaka kweli liwe la uwakilishi wa wananchi wote, lazima kuwaingiza wafanyakazi wa kawaida wake kwa waume katika mchakato wa kutoa uamuzi.


Itaendelea Jumanne Ijayo

CHANZO MWANASPORT GAZETI.

No comments:

Post a Comment