Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Thursday, 1 May 2014

TFF YATEUA WAKILI KUCHUNGUZA USAJILI WA DOMAYO AZAM FC

Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
KUTOKANA na tukio lililotokea jana (Aprili 30 mwaka huu) kwenye kambi ya timu ya Taifa (Taifa Stars) iliyopo Tukuyu mkoani Mbeya likihusisha usajili wa baadhi ya timu, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemteua Wakili Wilson Ogunde kuchunguza mlolongo mzima wa tukio hilo.
Taarifa ya TFF kwa BIN ZUBEIRY leo asubuhi imesema kwamba, baada ya kukamilisha uchunguzi wake, Wakili Ogunde ataishauri TFF kuhusu hatua za kisheria na kikanuni za kuchukua.

Frank Domayo akisaini Azam FC jana
TFF imesema katika taarifa yake inatoa wito kwa wachezaji, klabu na wadau wa mpira wa miguu kufuata kanuni na taratibu katika utendaji wao.
Viongozi wa Azam FC jana walikwenda kwenye kambi ya Taifa Stars kukamilisha taratibu za usajili na kiungo Frank Domayo, aliyemaliza Mkataba wake Yanga SC.
Baada ya kufanikiwa kumsainisha Mkataba wa miaka miwili, wasimamizi wa kambi waliwaitia Polisi viongozi wa Azam FC ambao hata hivyo baadaye waliachiwa. Lakini inadaiwa fomu za usajili zilichanwa.
Azam si klabu ya kwanza kusajili mchezaji katika kambi ya timu ya taifa, kwani vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga ndiyo waasisi wa mchezo huo.
Mwaka jana Simba SC walisaini Mkataba mpya na kiungo wao, Amri Kiemba akiwa katika kambi ya Taifa Stars, hoteli ya Tansoma mjini Dar es Salaam.

Inaruhusiwa kwa wakubwa tu; Kiongozi wa Yanga SC, Seif Ahmed 'Magari' alimtoa kambi ya Taifa Stars, beki Kevin Yondan akiwa Simba SC na kumsainisha mwaka 2012.

Yanga SC iliwasajili Domayo kutoka JKT Ruvu, Kevin Yondan kutoka Simba SC wote wakiwa katika kambi ya Taifa Stars Dar es Salaam miaka miwili iliyopita.

CHELSEA NJE ULAYA, YAPIGWA 3-1 DARAJANI...FAINALI NI ATLETICO NA REAL MADRID

CHELSEA imeaga Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufungwa mabao 3-1 na Atletico Madrid ya Hispania usiku huu Uwanja wa Stamford Bridge, London.
Atletico sasa itakutana na jirani zao, Real Madrid katika fainali mwezi ujao nchini Ureno, ambao jana waliwang’oa mabingwa watetezi, Bayern Munich kwa 4-0 mjini Munich na kufanya ushindi wa jumla wa 5-0.

Heshima sasa; Diego Costa kushoto akishangilia na mchezaji mwenzake, Koke baada ya kufunga bao la pili



Fernando Torres alitangulia kuifungia Chelsea dakika ya 36 kwa pasi ya Azpilicueta baada ya kazi nzuri ya Willian, lakini Adrian Lopez akaisawazishia Atletico dakika ya 44 kwa pasi ya Juanfran.
Diego Costa akafunga bao la pili kwa penalti dakika ya 61 kabla ya Arda Turan kumaliza kazi dakika ya 72 na Atletico imefuzu kwa ushindi wa jumla wa 3-1 baada ya sare ya 0-0 katika mchezo wa kwanza Madrid wiki iliyopita.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Jose Mourinho dakika ya 54 kumtoa beki Ashley Cole na kumuingiza mshambuliaji Samuel Eto’o ndiyo yaliigharimu Chelsea. Eto’o ndiye aliyesababisha penalti iliyofungwa na Costa.

Wednesday, 30 April 2014

MAYWEATHER AONYESHA JEURI YA FEDHA, SASA ATAKA KUNUNUA TIMU MAREKANI

KAMA anavyotamba katika ngumi za kulipwa hadi sasa akiwa hajapoteza pambano licha ya kupigana na mabondia wakali duniani, Floyd Mayweather anataka kununua klabu ya mpira wa kikapu Marekani, inayomilikiwa na milionea anayekabiliwa na kashfa ya ubaguzi.
Hakuna ajabu kwa mkali huyo wa kutupa mikono kwenye miili ya wenzake, anayekwenda kwa jina la utani Money Mayweather juu ya hilo, kwa sababu ana uwezo kifedha.
Floyd Jnr anataka kutoa dola za Kimarekani Milioni 40 ambazo ni sehemu tu ya pato lake la pambano la Jumamosi wiki hii, atakalolipwa dola bilioni 1.8 ili kuinunua Los Angeles Clippers.
Mutu ya fweza: Floyd Mayweather akiwasili ukumbi wa MGM Grand kuelekea pambano lake na Marcos Maidana

Kuhusu Marcos Maidana, Muargentina anayetarajiwa kupambana naye mjini Las Vegas, Mayweather amesema: "Amekuwa babu kubwa katika mapambano yake manne yaliyopita. Ana wastani wa asilimia 80 ya Knockout (KO). Hivyo siwezi kumdharau huyu jamaa,".
Kuhusu Clippers, ambayo mmiliki wake Donald Sterling amefungiwa maisha kujihusisha na masuala ya mpira wa kikapu baada ya kupatikana na hatia ya kuwatolea maneno ya kibaguzi watu weusi wa timu yake wakiwemo wachezaji, Mayweather amesema: "Ninataka kuinunua Clippers? Ndiyo. Naweza kuwaunganisha pamoja watu ambao watakuwa tayari.
"Kununua timu ya Ligi Kuu ya kikapu ni kitu fulani ambacho nataka kuongeza katika kampuni yetu inayokua kwa kasi ya Mayweather Promotions, ambayo sasa si kwa ajili ya ngumi tu, bali tunajihusisha pia na mavazi, muziki na sinema,"alisema.


Kifungo cha maisha: Mmiliki wa Los Angeles Clippers, Donald Sterling hawezi kujihusisha na masuala ya mpira wa kikapu baada ya kutoa kauli ya kibaguzi hadharani

KATIBU MKUU WA FIFA AWASILI KESHO DAR

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Jerome Valcke anawasili nchini kesho (Mei 1 mwaka huu) ambapo atafungua semina ya mawasiliano kwa nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Valcke ambaye atafuatana na maofisa wengine saba wa FIFA baadaye kesho hiyo hiyo (Mei 1 mwaka huu) atakuwa na mkutano na waandishi wa habari. Mkutano huo utafanyika saa 4 kamili asubuhi kwenye hoteli ya Double Tree by Hilton iliyopo Oysterbay, Dar es Salaam.

Sunday, 27 April 2014

MADOGO WA NGORONGORO WALIVYOWATOA WAKENYA JANA NA KUJIWEKA KWA NIGERIA


Kiungo wa timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes, Mudathir Yahya akimtoka kiungo wa Kenya katika mchezo wa jana kuwania tiketi ya Fainali za Afrika nchini Senegal mwakani. Tanzania iliitoa Kenya kwa penalti 4-3 baada ya sare ya jumla ya 0-0. Ngorongoro sasa itamenyana na Nigeria katika hatua inayofuata.


Kevin Friday wa Tanzania akimuacha chini beki wa Kenya

Wachezaji wa Tanzania wakishangilia baada ya mechi


Ally Bilal wa Tanzania akimtoka Hillary Dan wa Kenya


Mange Chagula wa Tanzania kushoto akigombea mpira na Hillary Dan wa Kenya aliye tayari kusaidiwa na wenzake


Kipa wa Kenya, Farouk Shikhalo akidaka mpira huku akilindwa na beki wake, Hillary Dan aliye mbele ya Ally Bilal wa Tanzania

Kevin Friday wa Tanzania kulia akimtoka Victor Ndinya wa Kenya

Mange Chagula wa Tanzania akiteleza na mpira mbele ya Evans Makari wa Kenya

Iddi Suleiman wa Tanzania akiwatoka mabeki wa Kenya

Iddi Suleiman wa Tanzania akimuacha chini beki wa Kenya

Benchi la Ufundi la Tanzania wakati wa penalti jana