Na Baby Akwitende, Dar es Salaam
MASHINDANO ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame yamepangwa kufanyika kuanzia Agosti 9 hadi 23 mwaka huu jijini Kigali nchini Rwanda.
Tanzania Bara itawakilishwa na Yanga katika mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati ( CECAFA).
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana , Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, alisema timu zote wanachama wa shirikisho hilo zinatarajiwa kushiriki.
Kikosi cha Yanga SC
Musonye alisema kuwa bado sekretarieti haijateua timu mwalikwa katika mashindano hayo kutokana na mabadiliko ya kalenda ya michuano hiyo ambayo hufanyika kila mwaka kati ya mwezi Mei na Juni.
"Ratiba kamili ya mashindano hayo itatolewa baadaye", alisema Musonye.
Mlezi wa CECAFA na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ameshathibitisha kutoa zawadiambayo ni Dola za Marekani 60,000 ambazo alianza kutoa tangu mwaka 2002.
Wadhamini wengine waliothibitisha kudhamini mashindano ya mwaka huu ni kituo cha televisheni cha Super Sport.
Bingwa mtetezi wa mashindano hayo ni Atraco ya Burundi na mfungaji bora wa michuano hiyo alikuwa ni Amissi Tambwe, anayeichezea Simba akitokea kwa mabingwa hao.