Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Wednesday, 9 April 2014

YANGA SC YAIPUMULIA AZAM FC KILELENI, BINGWA MWAKA HUU ATAKUWA BINGWA KWELI

Na Renatus Mahima, Dar es Salaam
YANGA SC imepunguza pengo la pointi inazozidiwa na vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Azam FC hadi kubaki pointi moja, kufuatia kuibwaga Kagera Sugar ya Bukoba mabao 2-1 jioni hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yanaifanya timu hiyo inayofundishwa na babu Mholanzi, Hans van der Pluijm kutimiza pointi 52, baada ya kucheza mechi 24, wakati Azam FC iliyocheza mechi 23 ina pointi 53 kileleni.
Hamisi Kiiza ‘Diego’ aliifungia Yanga SC bao la kwanza dakika ya tatu, akiunganisha krosi maridadi ya Mrisho Ngassa.

Hamisi Kiiza aliifungia Yanga bao la kwanza dakika ya tatu tu

Didier Kavumbangu aliifungia Yanga SC bao la pili dakika 36 akimlamba chenga kipa Agatony Anthony baada ya kupokea krosi nzuri ya Simon Msuva na kuituliza kifuani kwanza, kabla ya kumtesa kipa wa timu ya Bukoba.
Sifa zimuendee Mrisho Ngassa kwa bao hilo, kwani ndiye aliyeanzisha shambulizi hilo kwa kuwatoka wachezaji wa Kagera na kumchomekea Simon Msuva mpira kwenye njia akapiga krosi.
Hilo lilikuwa bao la 30 katika mashindano yote kwa Kavumbangu ndani ya mechi 60 alizoichezea Yanga SC katika misimu miwili. Msuva naye amecheza mechi ya 30 leo akijivunia kutoa krosi ya bao.
Beki Ernest Mwalupani alikuwa mwenye bahati kwa kuonyeshwa kadi ya njano dakika ya 64 na refa Maalim Abbas wa Rukwa akimtuhumu kuwapendelea wenyeji katika kosa ambalo lilistahili kadi nyekundu.
Daudi Jumanne aliifungia Kegara Sugar bao la kufutia machozi dakika ya 62 kwa shuti kali.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Frank Domayo, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Didier Kavumbangu, Mrisho Ngassa/Hussein Javu dk63 na Hamisi Kiiza/Nizar Khalfan dk86.
Kagera Sugar; Agatony Anthony, Salum Kanoni, Mohamed Hussein, Ernest Mwalupani, Maregesi Mwangwa, George Kavilla, Benjamin Asukile/Juma Mpola dk55, Daudi Jumanne, Adam Kingwande/Zuberi Dabi dk61, Themi Felix/Hamisi Kitaganda dk84 na Paul Ngway.
Kutoka Mlandizi, Pwani mchezo kati ya wenyeji Ruvu Shooting na Azam FC ya Dar es Salaam uliokuwa ufanyike jioni ya leo Uwanja wa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani umeahirishwa hadi kesho kufuatia mvua kubwa.
Timu hazikuwahi hata kuingia uwanjani kupasha misuli moto kutokana na mvua kubwa na Uwanja kujaa maji na ilipowadia Saa 10:20 waamuzi wa mechi hiyo waliingia uwanjani kukagua na kuvunja mchezo.
Kilifuatia kikao cha pande zote nne, baina ya viongozi wa Ruvu na Azam pamoja na TFF na marefa ambao waliafikiana mechi ichezwe kesho iwapo hali itakuwa nzuri.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ alikuwepo na kushuhudia hali hiyo.
Isihaka Shirikisiho wa Tanga ndiye aliyetarajiwa kuwa refa wa mchezo wa leo, akisaidiwa na Hassan Zani na Agness Pantaleo wote wa Arusha na refa wa akiba mwenyeji, Simon Mbelwa.
Azam yenye pointi 53 itaendelea kuishi kileleni mwa Ligi hata Yanga SC inayocheza na Kagera Sugar hivi sasa mjini Dar es Salaam itashinda, kwani wana Jangwani hao watatimiza pointi 52 huku pia wakiwa wamecheza mechi moja zaidi

BAYERN MUNICH YAING'OA MAN UNITED, BARCELONA NAYO YATUPWA HUKO KWA WASIOJUA

MANCHESTER United ya England imeaga Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufungwa mabao 3-1 na wenyeji Bayern Munich Uwanja wa Allianz-Arena mjini Munich, Ujerumani usiku huu.
Hiyo inamaanisha United imeaga kwa kipigo cha jumla ya mabao 4-2, baada ya awali kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 Uwanja wa Old Trafford mjini Manchester.
United leo ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 57, mfungaji beki wake Mfaransa, Patrice Evra aliyefumua shuti kali kwa guu la kushoto baada ya kupokea pasi ya Antonio Valencia.


Sekunde 22 baadaye Mcroatia Mario Mandzukic akaisawazishia Bayern akitumia fursa ya wachezaji wa United kuzubaa kwa furaha ya bao, wakidhani biashara imekwisha na kumbe mpira ni hadi filimbi ya mwisho.

Tuesday, 8 April 2014

112 WAFANIKIWA KUINGIA HATUA YA PILI KATIKA MASHINDANO YA KUSAKA VIPAJI VYA UIGIZAJI TANZANIA


Majaji wa Shindano la Kusaka la Vipaji vya Uigizaji Tanzania lijulikanalo kama Tanzania Movie Talents wakijadiliana jambo wakati wa Zoezi la kusaka vipaji vya uigizaji kuingia Hatua ya pili kwa washiriki waliofanikiwa kupita kwenye mchujo.Kulia ni Single Mtambalike (Rich Rich), Ivon Chery (Monalisa) na Roy Sarungi.

Washiriki waliofanikiwa kuingia kwenye hatua ya pili wakifanyiwa usaili kwaajili ya hatua ya pili sasa

Muongozaji wa Mradi wa Shindano la Kusaka Vipaji vya Kuigiza Tanzania lijulikanalo kama Tanzania Movie Talents, Bw Stanford Kihole (kulia) akitoa maelekezo kwa washiriki waliofanikiwa kuingia hatua ya pili katika mashindano ya kusaka vipaji vya uigizaji Tanzania likiwa limeaingia hatua ya pili Mkoani Mwanza

ROONEY FITI KABISA, AWAPASHIA KIKAMILIFU BAYERN MUNICH LEO

MSHAMBULIAJI Wayne Rooney amerejesha matumaini ya Manchester United kutinga Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuanza mazoezi kwa ajili Robo Fainali ya pili dhidi ya mabingwa watetezi, Bayern Munich Uwanja wa Allianz Arena kesho.
Rooney alikosa mechi ya Ligi Kuu England United ikiifunga mabao 4-0 Newcastle mwishoni mwa wiki kutokana na maumivu ya mguu, lakini sasa kuna uwezekano kesho akacheza
Ryan Giggs pia alifanya mazoezi baada ya kukosa mechi dhidi ya Newcastle, lakini Marouane Fellaini, ambaye alitolewa nje Uwanja wa St James Park baada ya kuumia na Rafael hawakushiriki mazoezi leo.
Baada ya sare ya 1-1 nyumbani, United sasa wanatakiwa kushinda ugenini dhidi ya Bayern ili kutinga Nusu Fainali.

Mazoezi makali: Rooney akifanya mazoezi kuelekea mchezo wa marudiano na Bayern Munich

AZAM NA YANGA KATIKA WIKI YA VITA KALI UBINGWA WA BARA

Na Boniface Wambura, Dar es Salaam
LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaendelea kesho (Aprili 9 mwaka huu) huku timu za Azam na Yanga ambazo zipo nafasi mbili za juu zikiendelea kuchuana.
Azam itakuwa mgeni wa Ruvu Shooting katika mechi itakayochezwa kwenye Uwanja wa Mabatini uliopo Mlandizi mkoani Pwani. Nayo Yanga itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar katika Uwanja wa Taifa jijini.
Yanga, Azam, Ruvu Shooting na Kagera Sugar zote zimeshinda mechi zao za raundi ya 23 wakati mechi za kesho zitakuwa kwa ajili ya kukamilisha raundi ya 24 ya ligi hiyo ambayo inatarajia kukamilika Aprili 19 mwaka huu.

Yanga na Azam kesho zinaingia katika wiki ngumu ya kusaka ubingwa

Ligi hiyo itaingia raundi ya 25 Aprili 12 na 13 mwaka huu ambapo timu zote 14 zitakuwa viwanjani. Aprili 12 mwaka huu itakuwa Mtibwa Sugar vs Ruvu Shooting (Manungu, Morogoro), Coastal Union vs JKT Ruvu (Mkwakwani, Tanga), na Tanzania Prisons vs Rhino Rangers (Sokoine, Mbeya).

Monday, 7 April 2014

FIFA YAITANGAZIA NEEMA TANZANIA, TAYARI IMEIPA DOLA MILIONI 6 TFF

Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
TANZANIA itanufaika na msaada mkubwa kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), wenye la kuboresha soka ya nchi hiyo na nyingine zote za Afrika, imesema taarifa ya FIFA.
Akizungumza wakati wa kufunga semina ya siku tatu mjini Johannesburg, Afrika Kusini Alhamisi, ambayo ilihudhuriwa na wajumbe kutoka nchi 26 wanachama wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke ametoa ahadi ya kuipa sapoti kubwa soka ya Afrika ili siku moja timu zake ziweze kucheza Fainali ya Kombe la Dunia.


Washiriki wa semina ya siku tatu ya FIFA mjini Johannesburg, Afrika Kusini wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa kufunga semina hiyo Alhamisi
Chini ya Mtendaji Mkuu wa Fainali za Kombe la Dunia 2010 na Rais wa Shirikisho la Soka Kenya (SAFA), Danny Jordaan, semina hiyo ambayo ilimalizika Alhamisi, ilifikia makubaliano ya kuongeza umakini katika kuboresha mambo mbalimbali, ikiwemo kiwango cha soka, utawala bora na kutatua matatizo yote sugu katika soka ya Afrika kwa msaada wa FIFA.
“Programu zote ambazo tutajadili kwenye hii semina, tunaweza kuwahakikishia kuwa hadi kufika mwaka 2022 mambo yatakuwa safi, na hii ni kwa mshikamano wa pamoja baina yetu,”alisema Valcke na kuongeza; “Tutahakikisha mnaimarika na kusonga mbele, ambayo itafanya ligi zenu ziwe bora, mtaendeleza mradi wa soka za vijana kwa kila mmoja anayetaka kucheza soka Afrika. Tutakusaidieni ili muwe bora, na tunataka timu za Afrika muda si mrefu zifike fainali ya Kombe la Dunia la FIFA.”
Kwa upande wake, Suketu Patel, Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (COSAFA) na Makamu wa Rais wa CAF, ameishukuru FIFA na kuzitaka nchi za Afrika kuonyesha bidii ya kusaka maendeleo. “Lazima tuwashukuru FIFA,” alisema na kuongeza. “Kila nchi mwanachama (wa FIFA) amepata kiasi cha dola (za Kimarekani) Milioni 6 kwa muongo uliopita. Sasa tujiulize tumefanyia nini kwa fursa hiyo ambayo tumekuwa tukipewa? Tumeitumia kuboresha miundombinu, au hali bado ni ile ile kama ilivyokuwa kabla ya misaada hii?,”alihoji.
Marais, Makatibu Wakuu na Wakurugenzi wa Ufundi wa vyama na mashirikisho ya soka wanachama wa CAF walihudhuria semina hiyo kutoka nchi za Angola, Botswana, Misri, Eritrea, Ethiopia, Gambia, Ghana, Kenya, Lesotho, Liberia, Lybia, Malawi, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Shelisheli, Sierra Leone, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Swaziland, Tanzania, Uganda, Zambia, Zimbabwe na wenyeji Afrika Kusini.

ADEBAYOR AIREJESHA SPURS JUU YA MAN UNITED ENGLAND

TOTTENHAM Hotspur imerudi nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu ya England kufuatia ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Sunderland usiku wa jana Uwanja wa White Hart Lane, London.
Emmanuel Adebayor alifunga mabao mawili na mengine yakafungwa na Kane, Eriksen na Sigurdsson, wakati bao la kufutia machozi la Sunderland lilifungwa na Cattermole.
Ushindi huo unaifanya Spurs itimize pointi 59 baada ya kucheza mechi 33 na kurejea nafaasi ya sita, ikiishuaha Manchester United kwa nafasi moja hadi ya saba. United imekusanya pointi 57 katika mechi 33.

Mtu muhimu: Adebayor akikimbia kushangilia jana baada ya kuifungia Spurs

NGORONGORO HEROES KUPAMBANA NA AFRIKA KUSINI IKIITOA KENYA

Na Boniface Wambura, Dar es Salaam
TIMU ya soka ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20, Ngongoro Heroes imerejea nchini leo mchana (Aprili 7 mwaka huu) kutoka Kenya mechi ya michuano ya Afrika dhidi ya wenyewe, na itaingia kambini Alhamisi.
Ngorongoro Heroes ambayo imewasili saa 8.25 kwa ndege ya Kenya Airways ilitoka suluhu na Kenya katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Kanyetta uliopo katika mji wa Machakos.

Kipa wa Ngorongoro, Aishi Manula

Kocha John Simkoko amesema benchi lake la ufundi linafanyika kazi upunguzi uliojitokeza ili wafanye vizuri kwenye mechi ya marudiano itakayochezwa Aprili 27 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Iwapo Ngorongoro Heroes itaitoa Kenya, raundi inayofuata itacheza na Afrika Kusini. Fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 20 zitafanyika mwakani nchini

TFF YAIPONGEZA TIMU YA WATOTO WA MITAANI KUTWAA UBINGWA WA DUNIA

Na Boniface Wambura, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limeipongeza timu ya Tanzania ya Watoto wa Mitaani kwa kutwaa ubingwa wa Dunia wa Watoto wa Mitaani baada ya jana (Aprili 6 mwaka huu) kuifunga Burundi mabao 3-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa jijini Rio de Janeiro, Brazil.
TFF imesema ushindi wa timu hiyo ni fahari kwa Tanzania, lakini kubwa ni kwa kituo cha Mwanza ambacho ndicho kinachoiendesha pamoja na wadhamini na wafadhili walioiwezesha kushiriki fainali hizo kwa mara ya pili mfululizo.

“Vilevile ushindi huo unatoa changamoto kubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kuwa watoto wa mitaani ni sehemu tu ya vipaji vilivyotapaa nchini, hivyo iliyopo ni kuvisaka na kuvibaini vipaji hivyo kwa ajili ya ustawi wa mchezo huo nchini,” imesema taarifa ya TFF.
TFF imeahidi kuendelea kushirikiana na kituo hicho cha Mwanza, na vingine vyote ambavyo vinajishughulisha na mchezo huu, lengo likiwa ni kuundeleza na hata kutoa ajira kwa vijana hapo baadaye kupitia mpira wa miguu.
Timu hiyo inarejea nchini Alhamisi (Aprili 10 mwaka huu) ambapo itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 10 jioni kwa ndege ya Emirates.
NA BIN ZUBERRY