Na Boniface Wambura, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limeipongeza timu ya Tanzania ya Watoto wa Mitaani kwa kutwaa ubingwa wa Dunia wa Watoto wa Mitaani baada ya jana (Aprili 6 mwaka huu) kuifunga Burundi mabao 3-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa jijini Rio de Janeiro, Brazil.
TFF imesema ushindi wa timu hiyo ni fahari kwa Tanzania, lakini kubwa ni kwa kituo cha Mwanza ambacho ndicho kinachoiendesha pamoja na wadhamini na wafadhili walioiwezesha kushiriki fainali hizo kwa mara ya pili mfululizo.
“Vilevile ushindi huo unatoa changamoto kubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kuwa watoto wa mitaani ni sehemu tu ya vipaji vilivyotapaa nchini, hivyo iliyopo ni kuvisaka na kuvibaini vipaji hivyo kwa ajili ya ustawi wa mchezo huo nchini,” imesema taarifa ya TFF.
TFF imeahidi kuendelea kushirikiana na kituo hicho cha Mwanza, na vingine vyote ambavyo vinajishughulisha na mchezo huu, lengo likiwa ni kuundeleza na hata kutoa ajira kwa vijana hapo baadaye kupitia mpira wa miguu.
Timu hiyo inarejea nchini Alhamisi (Aprili 10 mwaka huu) ambapo itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 10 jioni kwa ndege ya Emirates.
NA BIN ZUBERRY
No comments:
Post a Comment