Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Friday, 4 April 2014

CANNAVARO AINGIA KAMBINI YANGA SC TAYARI KWA MECHI NA JKT RUVU JUMAPILI

Na Renatus Mahima, Dar es Salaam
NAHODHA wa Yanga SC, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ jana ameingia kambini katika hoteli ya Kiromo, Bagamoyo, Pwani kujiunga na wenzake kwa ajili ya mchezo wa Jumapili dhidi ya JKT Ruvu.
Cannavaro alikuwa anaumwa Malaria tangu arejee kutoka Tanga mapema wiki hii, ambako mwishoni mwa wiki timu yake ilifungwa mabao 2-1 na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani.
Mganda, Emmanuel Okwi bado hajapatikana na viongozi wanalalamika hata simu yake haipatikani, wakati mgonjwa mwingine wa Malaria, kiungo Haruna Niyonzima naye bado anajiuguza nyumbani kwake.

Kapteni kambini; Nadir Haroub 'Cannavaro' ameingia kambini jana, lakini Okwi bado hapatikani

Beki Kevin Yondan ameondolewa katika programu ya mchezo ujao kwa kuwa anatumikia adhabu ya kadi mbili za njano na hayupo kambini na mchezaji mwingine ambaye sababu za kutokuwepo kwake kambini hazijulikani ni Athumani Iddi ‘Chuji’, ingawa watu wake wa karibu wanasema ana matatizo ya kifamilia.
Habari njema tu ni kwamba, makipa wote watatu waliosajiliwa msimu huu Yanga SC, Juma Kaseja, Deo Munishi ‘Dida’ na Ally Mustafa ‘Barthez’ wapo kambini na wanaendelea na mazoezi.
Baada ya kupoteza pointi tatu zinazowafanya waachwe mbali na kidogo na Azam FC katika mbio za ubingwa, Yanga SC itashuka dimbani Jumapili hii kumenyana na timu nyingine ya Jeshi la Kujenga Taifa, JKT Ruvu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Azam FC inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 53 baada ya kucheza mechi 23, ikifuatiwa na Yanga SC yenye pointi 46 za mechi 22 na Mbeya City yenye pointi 45 za mechi 23 ni ya tatu.
Wakati Yanga SC itacheza na JKT Ruvu Jumapili Uwanja wa Taifa, Mbeya City itacheza na Ashanti United Jumamosi Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Azam FC ilikuwa icheze na Ruvu Shooting Jumapili hii pia, Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani lakini mchezo huo umesogezwa mbele hadi Aprili 9, kutokana na timu hiyo kuwa na wachezaji wengi katika kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes.
Ngorongoro Heroes ipo Nairobi, Kenya tangu jana kwa ajili ya mechi ya kuwania kucheza Fainali za Vijana Afrika, itakayochezwa Jumapili ya Aprili 6 mwaka huu Uwanja wa Machakos ulioko kilometa 80 kutoka jijini Nairobi na Azam ina wachezaji zaidi ya watano kwenye kikosi hicho.
Hao ni Aishi Manula, Bryson Raphael, Gardiel Michael, Kevin Friday, Mudathir Yahya, Farid Mussa na Hamad Juma.

No comments:

Post a Comment