Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Monday, 31 March 2014

WAHABESHI WAMZUIA KOCHA MPYA STARS KUJA DAR

Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
KOCHA mpya wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mholanzi Martinus Ignatius ‘Mart’ Nooij sasa atawasili mwishoni mwa mwezi huu badala ya leo kama ilivyotarajiwa, imefahamika.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi aliahirisha Mkutano na Waandishi wa Habari uliokuwa ufanyike Machi 24 mwaka huu kumtaja rasmi mwalimu huyo, ili zoezi hilo lifanyike atakapowasili- na sasa atalazimika kusubiri hadi kuanzia Aprili 20.

Kocha ambaye wa Stars Mart Nooij aliyekuwa awasili leo, sasa anatarajiwa kutua nchini kuanzia Aprili 20, mwaka huu

Hiyo inafuatia klabu yake, St George ya Ethiopia kumbana asiondoke hadi itakapopata mwalimu mpya, zoezi ambalo Nooij anaisaidia timu hiyo kuhakikisha inapata kocha mwingine bora.
BIN ZUBEIRY inafahamu tayari Nooij amekwishasaini Mkataba wa miaka miwili na TFF- ingawa sasa ujio wake unakumbwa na mizengwe.
Ulikuwa mchakato makini, uliohusisha wataalamu na washauri wa kimataifa juu ya masuala ya ufundi ya soka ambao umefanikisha kupatikana mwalimu huyo wa Kiholanzi aliyezaliwa Julai 3, mwaka 1954 mjini Beverwijk, Uholanzi.
Nooij amewahi kuwa mwalimu maalum katika programu za maendeleo ya soka katika Chama cha Soka Uholanzi (DFA) na pia amewahi kufundisha timu ya EVC 1913 ya Marekani na baadaye Kazakhstan.
Alikuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Burkina Faso katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2003 na mwaka 2004 alikuwa kocha wa muda wa klabu ya FC Volendam ya Uholanzi.
Mwaka 2007 aliteuliwa kuwa kocha wa Msumbiji na akaiwezesha kufuzu kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2010, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza Mambas wanashiriki AFCON baada ya msoto wa miaka 12.
Hata hivyo, katika fainali hizo, Msumbiji ilishika mkia katika kundi lake baada ya kuambulia sare moja na kufungwa mechi mbili. Baada ya kukosa tiketi ya AFCON 2012, Nooij akajiuzulu Septemba mwaka 2011 na nafasi yake kuchukuliwa na Mjerumani, Gert Engels.
Aprili 19 mwaka 2012, aliajiriwa na klabu ya Santos ya Afrika Kusini, ambako hata hivyo alifukuzwa Desemba 18, mwaka 2012 na kunyakuliwa na St George ya Ethiopia anakoendelea na kazi hadi sasa.
Baada ya kusaini Mkataba wa miaka miwili na TFF kuja kuifundisha Stars, Nooij anasubiri barua maalum ya kuruhusiwa kuondoka baada ya kukamilisha taratibu za kuvunja Mkataba uliokuwa unaelekea ukingoni na klabu hiyo ya Addis Ababa.

No comments:

Post a Comment