Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Saturday 11 January 2014

NINA WASIWASI YANGA WANAUVAGAA MKENGE KWA PLUIJM

YANGA SC inasaka kocha Mkuu, baada ya kumfukuza Mholanzi Ernie Brandts mwishoni mwa mwaka na kuna uwezekano ikaangukia kwa Mholanzi mwingine, Johannes Franciscus ‘Hans’ van der Pluijm.
Habari za ndani kutoka Yanga zinasema, imemuita kwa mazungumzo, kocha huyo, aliyewahi kuifundisha Berekum Chelsea ya Ghana na anaweza kutua leo Dar es Salaam iwapo atafanikiwa kupata ndege.
Hakupata usafiri wa ndege kutoka Ghana kuja Dar es Salaam jana na ikaelezwa alikuwa anahaha kutafuta ndege ya kuunganisha na kama akifanikiwa basi atakuja nchini leo, ikishindana wakati wowote mapema wiki ijayo.


Pluijm anakuja kufanya mazungumzo na Yanga, baada ya uongozi wa klabu hiyo kuridhishwa na wasifu wake katika orodha ndefu ya walimu zaidi ya 30 walioomba kazi Jangwani.
Kuna wasiwasi mkubwa juu ya namna mchakato huu ulivyoendeshwa hadi katika waombaji zaidi ya 30, ikaonekana Pluijm ndiye anafaa. Vigezo vipi walitumia Yanga? Sijui. Wakati wa kutafuta mwalimu, mambo ya kuzingatia ni rekodi yake, elimu yake, uwezo wa kufanya kazi na si vibaya ukatazama na uzoefu pia.
Kocha mzuri ni ambaye ameshinda mataji, ikibidi kushinda tuzo yeye mwenyewe binafsi na asiye na rekodi ya kufukuzwa fukuzwa, zaidi ya hapo mwenye elimu nzuri ya ufundishaji mpira, aliyesomea katika vyuo vyenye kuheshimika na kupewa leseni za bodi kubwa za soka kama UEFA.
Niwapongeze Simba SC, wamepata kocha mzuri, Zdravko Logarusic raia wa Croatia ambaye alipokuwa Kenya aliiwezesha Gor Mahia kushinda mataji na yeye mwenyewe kushinda tuzo. Ana elimu nzuri na ana leseni ya UEFA. Ni vitu rahisi tu.
Chanzo cha habari juu ya ujio wa Pluijm kilisema walivutiwa na mwalimu huyo kwa sababu alipokuwa Berekum Chelsea alizifunga TP Mazembe na Al Ahly. Kwao hilo, Yanga wameridhika na wamemualika kwenye mazungumzo ya Mkataba.
Ukweli ni kwamba Yanga wanatakiwa kutulia sana katika suala la uteuzi wa mwalimu- na wafanye uchunguzi wa kina. Yanga lazima wajue kwa undani, n kweli Pluijm alikuwa chachu ya mafanikio ya Berekum wakati huo, au kulikuwa kuna mtu nyuma yake? Na mbona hakudumu katika timu hiyo alifukuzwa baada ya muda mfupi. Inakuwaje kocha mzuri aliyeleta mafanikio katika timu akafukuzwa?
Historia ya Franciscus Johannes ‘Hans’ van der Pluijm inasema alizaliwa Januari 3 mwaka 1949 na alianzia kwenye kucheza soka akiwa kipa.
Enzi zake aliidakia kwa miaka 28 klabu ya FC Den Bosch akicheza mechi 338 ndani ya misimu 18 na alipostaafu baada ya kuumia goti akawa kocha wa timu hiyo.
Alianza vyema ukocha akiiwezesha FC Den Bosch kutwaa ubingwa wa Daraja la Kwanza na kupanda Ligi Kuu na ndiye aliyempa nafasi ya kwanza mshambuliaji Ruud van Nistelrooy akiwa kinda wa miaka 17 tu kucheza kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Aprili mwaka 1995, alisaini Mkataba wa miaka miwili na SBV Excelsior kabla ya kutimuliwa Januari 1997 na nafasi yake ikachukuliwa na Msaidizi wake, John Metgod.
Hiyo ilifuatia timu hiyo ya Rotterdam kushinda mechi mbili tu na sare tatu katika mechi 17 za msimu mzima.
Baada ya kuboronga Ulaya, ndipo akahamia Afrika mwaka 1999, alipokwenda kufundisha Ashanti Gold SC ya Ghana, akianza na Mkataba wa mwaka mmoja.
Ajax ya Uholanzi ikanunua hisa katika klabu hiyo Ijumaa ya Juni 18, mwaka 1999 asilimia 51 naye akatupiwa virago na kuhamia Saint-George SA ya Ethiopia kabla ya mwaka 2010 kujiunga na B-juniors Feyenoord ya Ghana, ambayo ni tawi la timu hiyo ya Rotterdam.
Mwaka 2012 alijiunga na Berekum Chelsea ambako pia alifukuzwa mwaka jana na kuhamia Medeama ya Ghana pia ambako nako alifukuzwa baada ya mechi saba tu, kufuatia matokeo mabaya mwanzoni mwa msimu, akivuna pointi nane kati ya 21.
Huu ndio wasifu wa kocha ambaye Yanga wanataka kumpa mkataba kati ya walimu zaidi ya 30 walioomba kazi. Niwe wazi mapema, nina shaka na mwalimu huyu kwa sababu tu ya hii rekodi yake, achilia mbali umri wake mkubwa ambao wazi hautumuwezesha kuhimilii mikiki.
Mei 8, mwaka jana Sir Alex Ferguson aliyezaliwa Desemba 31, mwaka 1941 alistaafu kufundisha soka akiwa Manchester United, akiwa ana umri wa miaka 72, lakini vuguvugu la kustaafu kwake lilianza tangu mwanzoni mwa muongo uliopita.
Yanga wanataka kuajiri kocha mwenye umri wa miaka 65, soka yenyewe hii ya Tanzania na aina ya wachezaji tulionao, kweli huo ni uamuzi sahihi? Nawasihi viongozi wa Yanga, warudi mezani watafakari tena uamuzi wao na pia wazingatie vigezo vya kitaalamu katika zoezi hilo, kwa sababu wakiboronga watapoteza muda tena.

No comments:

Post a Comment