Sunday, 5 January 2014
Azam: Kombe la Mapinduzi letu tena
NA MWANDISHI WETU
Baada ya timu yao kufuzu kucheza hatua inayofuata ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi, benchi la ufundi la Azam FC limesema ‘muziki’ wao ndiyo kwanza umeanza kunoga huku wakiahidi kutwaa taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo.
Azam, walio chini ya kocha mpya, Mcameroon Joseph Omog baada ya kusitisha mkataba na Muingereza Stewart Hall, wamekuwa timu ya kwanza kutinga hatua robo fainali ya mashindano hayo, baada ya kuifunga Tusker FC ya Kenya bao 1-0, katika mchezo wao wa pili wa Kundi B uliochezwa kwenye Uwanja wa Amaan visiwani hapa usiku wa kuamkia jana.
Akiitendea haki pasi murua ya Waziri Salum, mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Kipre Tchetche, ambaye alikuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, aliyepeleka kilio kwa wanafainali hao wa Kombe la Mapinduzi mwaka jana – Tusker, baada ya bao la shuti kali la mguu wa kulia dakika mbili kabla ya mapumziko. Bao ambalo lilidumu kwa dakika zote 90 zachezo huo ulioshuhudiwa na makocha kibao wa timu zinazoshiriki mashandno hayo wakiwamo Abdallah ‘King’ Kibadeni wa Ashanti United na Zdravko Logarusic wa Simba.
Ushindi huo uliifanya Azam, ambayo leo usiku inacheza mchezo wake wa mwisho wa Kundi C dhidi ya ‘wauza mitumba wa Ilala’, Ashanti United, ifikishe pointi sita baada ya kucheza michezo miwili wakati Tusker, inayocheza dhidi ya Spice Stars leo jioni, ilibaki na pointi zake tatu.
Akizungumza na NIPASHE mjini Unguja jana, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Kalimangonga Ongala alisema kikosi chao ndiyo kimeanza kuimarika na wanaamini kitafanya vizuri zaidi katika hatua inayofuata ya mashindano hayo, ambayo mwaka huu yanafanyika kwa mara ya nane tangu yaanzishwe 2006 kuazimisha Mapinduzi Tukufu ya Zanzibar.
“Likizo baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom inaonekana kuwaathiri wachezaji wengi wa kikosi chetu. Wamecheza vizuri mechi yetu ya pili dhidi ya Tusker, naona ndiyo tunaanza mashindano sasa,” alitamba Ongala.
“Tunamshukuru Mungu tumefuzu hatua inayofuata, lakini lazima tuhakikishe pia tunashinda mchezo wetu wa kesho (leo) dhidi ya Ashanti ili tumalize nafasi ya kwanza katika kundi letu,” alisema.
Lakini, Kocha wa Tusker FC, Francis Kimanzi aliliambia gazeti hili mjini Unguja jana kuwa, timu yake inaponzwa na maamuzi mabovu ya marefa wanaochezesha mashindano hayo mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment