Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Friday, 10 January 2014

AZAM FC YAVULIWA UBINGWA KOMBE LA MAPINDUZI, YAPIGWA 3-2 MBELE YA RAIS MWINYI AMAAN

Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
NDOTO za Azam FC kubeba kwa mara ya tatu mfululizo Kombe la Mapinduzi, leo zimeyeyuka baada ya kufungwa mabao 3-2 na KCC ya Uganda katika Nusu Fainali ya michuano hiyo Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Shujaa wa timu ya Watunza Jiji la Kampala leo alikuwa ni William Wadri aliyefunga bao la tatu dakika ya 45 na ushei, akiunganisha krosi ya Habib Kavuma.
Kabla ya hapo, Tony Odur aliifungia bao la kusawazisha KCC na kuwa 2-2 dakika ya 51, akiunganisha pia krosi ya Habib Kavuma.

Kipre Tchetche akimtoka mchezaji wa KCC katika mchezo wa leo

Kipa Mwadini Ali alidaka mechi zote nne za awali bila kufungwa hata bao moja, lakini leo amekubali kufungwa mabao matatu rahisi na KCC.
Hadi mapumziko, tayari Azam FC walikuwa mbele kwa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Joseph Lubasha Kimwaga yote dakika za 16 na 32.
Kinda huyo aliyepandishwa kutoka akademi ya Azam msimu huu, alifunga bao la kwanza kwa kichwa akiunganisha kona iliyochongwa na beki wa kulia Erasto Nyoni kutoka wingi ya kulia.
Bao la pili Kamwaga aliitokea krosi ya chini ya mshambuliaji hatari wa Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche kutoka kushoto na kuteleza nayo hadi nyavuni.


Mzee Mwinyi aliishuhudia Azam ikipigwa 3-2
Baada ya kupata bao hilo, Azam walionekana kutaka kuwadharau wapinzani wao, walioitumia vyema fursa hiyo kupata bao moja kabla ya mapumziko, lililofungwa na Ibrahim Kiiza dakika ya 37.

Kazi bure; Joseph Kimwaga akipongezwa na Himid Mao baada ya kufunga bao la pili, lakini mabao yake hayakuwa na faida leo

Kipindi cha pili, mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog kuwatoa wachezaji wote wa safu ya mbele Kipre Tchetche, Joseph Kimwaga na Brian Umony na kuwaingiza Muamad Ismail Kone, Ibrahim Mwaipopo na Farid Mussa yaliigharimu timu.
Wachezaji wote walioingia walishindwa kucheza vizuri kama waliotoka na ndipo KCC ilipoutumia mwanya huo kutoka nyuma na kushinda mechi.
Kwa matokeo hayo, KCC inasubiri mshindi wa mechi ya usiku kati ya Simba SC ya Dar es Salaam na URA ya Uganda pia ikutane naye katika fainali Jumatatu.
Mchezaji Joseph Kimwaga alikabidhiwa king’amuzi na rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi baada ya kutajwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ali, Erasto Nyoni, Malika Ndeule, David Mwantika, Aggrey Morris, Kipre Balou, Himid Mao, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Kipre Tchetche, Brian Umony na Joseph Kimwaga.

No comments:

Post a Comment