NA SOMOE NG`ITU
Boniface Mkwasa
Kocha mkuu wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga, Boniface Mkwasa, amekerwa na utovu wa nidhamu wa nyota wawili wa Kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza, hivyo kuhitaji kufanyika kikao na uongozi wa klabu hiyo ili kuwajadili.
Wachezaji hao wawili ndiyo pekee ambao hadi jana walikuwa hawajaripoti katika mazoezi ya timu hiyo inayojiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara na mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkwasa aliyetua rasmi Yanga wiki iliyopita akitokea Ruvu Shooting ya mkoani Pwani, alisema anakerwa na tabia hiyo na anataka kuona chini ya uongozi wake wachezaji wote wanaheshimu mikataba yao ya kujiunga na klabu hiyo.
Mkwasa alisema ni vyema kila mchezaji aliye mzima akahudhuria mazoezi kama ilivyopangwa ili kila mmoja awe fiti, tayari kuitumikia timu katika mechi za ligi na mashindano ya kimataifa yanayokuja.
"Nimepanga kukutana na viongozi kujadiliana kuhusiana na wachezaji hao wawili, umefika wakati wakuheshimu mikataba yao na ruhusa waliyopewa na viongozi, wakiendelea na tabia hii inaharibu programu ya timu na hawataweza kuwa kwenye kiwango cha ushindani kama wangehudhuria mazoezi kikamilifu," Mkwasa alieleza.
Aliongeza kuwa, hana taarifa rasmi za kutokuwapo kwa wachezaji hao ndiyo maana kati ya leo na kesho atazungumza na viongozi kuelewa ruhusa zao zilitakiwa kumalizika siku gani. Alisema kila mchezaji anatakiwa kuwa na nidhamu kwenye timu na kwake hakuna mchezaji bora.
"Wachezaji wote wana haki sawa kwangu, nafahamu nidhamu ndiyo silaha ya mafanikio katika mchezo wa soka," aliongeza Mkwasa ambaye alishawahi kuifundisha Yanga miaka ya nyuma.
Alisema leo timu hiyo inatarajia kuendelea na mazoezi yake jioni kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama jijini Dar es Salaam na baadaye ratiba hiyo itabadilika.
Mkwasa na Juma Pondamali ambaye ni kocha mpya wa makipa wamepewa mikataba ya miaka miwili kila mmoja baada ya uongozi wa Yanga kusitisha mkataba na Kocha Mkuu, Mholanzi Ernie Brandts na kisha kutimua msaidizi wake, Fredy Felix Minziro pamoja na benchi lote la ufundi.
Hata hivyo, uongozi wa klabu hiyo, umesema bado unaendelea na zoezi la kusaka kocha mkuu ambaye atatoka nje ya nchi.
Yanga ambayo ni vinara katika msimamo wa Ligi Kuu baada ya kuvuna pointi 28 katika raundi ya kwanza, itaanza mzunguko wa pili Januari 25 kwa kuivaa Ashanti United kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment