Saturday, 11 January 2014
SHULE MASHUHURI YA ETON KUENDELEZA MICHEZO TANZANIA
Picha na Urban Pulse
Imeandikwa na Freddy Macha
Mradi wa majaribio ya mwezi mmoja ulioandaliwa na Waingereza kuendeleza shule sita wilaya za Arusha na Moshi unatazamiwa kuanza wiki hii, ilitangazwa London, mwishoni mwa juma. Wanafunzi Nicolas Zafiriou (18), Ali Lyon(19) na Tom Pearson (18) wakiwa na kocha wao Glen Pierce. Watashirikiana kutoa ufundi wa mpira. Mradi huu unaosimamiwa na kampuni ya kitalii, Safari Hub na Chuo cha Eton wakisaidiana na Ubalozi wa Tanzania, Uingereza, unatuma Mkuu wa Mafunzo ya Michezo Eton, Bwana Glen Pierce na wanafunzi watatu waliomaliza kidato cha sita wanaotarajia kuingia vyuo vikuu baadaye mwakani. shughuli hii itasaidiwa na ushirikiano wa chuo cha michezo Arusha (Future Stars Academy) na shirika la ufadhili linalopigana kuondoa umaskini, (ACE Africa).
Akiongea katika tafrija ndogo iliyofanywa Ubalozini, London kuuaga msafara , Mkurugenzi Mkuu wa Safari Hub, bwana Dilip Navapurkar alisema iko haja ya kujenga ujuzi toka utotoni ili “kuhakikisha timu ya taifa ya Tanzania inafanya vizuri katika michuano ya Kombe la Afrika na Dunia na kufikia kiwango cha mafanikio tunayoyaona nchi nyingine mathalan Nigeria, Ghana, Afrika Kusini na Ivort Coast.”
Mkurugenzi wa kampuni ya utalii Safari Hub, Dilip Navapurkar aliyefanya bidii kuhakikisha mambo yanafanyika akielezea lengo la safari. Mwalimu Pierce mwenye uzoefu wa Miaka 27 chuo cha Eton aliwafundisha pia wajukuu wa Malkia Uingereza, William na Harry. Wanafunzi atakaoongozana nao ni Tom Pearson, 18 ( ulinzi) Nicholas Zafiriou, 18 (kiungo) na Ali Lyon, 19 (mshambuliaji ). Wamechaguliwa kwa kufanya vizuri katika michezo mbalimbali ukiwemo mpira waliocheza timu ya shule ya Eton. Eton ilianzishwa karne ya 15 na Mfalme Henry wa 6 na ni moja ya shule bora sana duniani. Mawaziri Wakuu 19 wa Uingereza (akiwemo Winston Churchill, Tony Blair, David Cameron na Meya wa Jiji la London, Boris Johnson) walisoma hapa. Wabunge, mawaziri, waandishi maarufu (George Orwell na Ian Fleming mtunzi wa visa vya James Bond) na watoto wa wafalme mbalimbali duniani vile vile wamesoma Eton.
John Collenette wa ACE Afrika -inayojaribu kuondoa umaskini Afrika Mashariki akieleza ushirikiano utakaofanywa kufanikisha shughuli Arusha na Moshi. Tafrija ya kuwaaga ilifanywa na Balozi Peter Kallaghe na Afisa Balozi, Amos Msanjila aliyewakaribisha Tanzania. Mbali na kutoa mafunzo ya michezo wageni wanatazamiwa kukutana na wanahabari Jumanne, kutembelea mbuga za wanyama, Zanzibar na kupanda mlima Meru, Arusha. Lengo la mradi huu ni safari au mradi mfupi na hatimaye kuendeleza mahusiano kati ya wanafunzi wa Tanzania na Eton. Iko siku “timu ya mpira ya Eton itafanya ziara Tanzania na hatimaye Watanzania pia kuitembelea Eton,” Bwana Navapurkar alisema.
Picha ya pamoja. Toka kushoto, Afisa Balozi, Amos Msanjila, Tom Pearson, Dilip Navapurkar, Balozi Peter Kallaghe, Ali Lyon, Nicolas Zafiriou, Glen Pierce na Yusufu Kashangwa wa kituo cha Biashara Ubalozini. Akihimiza umuhimu wa safari hii, Balozi Kallaghe aliwaambia wageni kwamba Watanzania wanapenda sana soka na kuwaahidi wageni kuwa watafaidi uzuri wa nchi watakapofika kama sehemu ya mafanikio ya kibiashara siku za mbeleni na kufurahia michezo Tanzania. Akijibu maswali ya wanahabari, Bwana Navapurkar alisema gharama za safari na vifaa vimetokana na michango ya watu binafsi na shule zinazopakana na Eton ambazo zimefikia shilingi milioni 61 na nusu. Mbali na mafunzo ya mpira wanafunzi Arusha na Moshi watapewa vifaa na kufundishwa maana ya nidhamu, elimu na michezo, aliongeza kocha Glen Pierce. “Watoto watakaopewa fursa hiyo ni wale tu watakaohudhuria shule,” alisisitiza.
Afisa Balozi (Minister Counsellor) Amos Msanjila akifanya mahojiano na Freddy Macha na Urban Pulse. Akisifia tabia ya Watanzania, Mkurugenzi wa Safari Hub, yenye makao Tanzania, Bwana Navapurkar, alisema Tanzania imechaguliwa shauri ni nchi yenye amani, demokrasia na utulivu wa kisiasa, ukilinganisha na nchi nyingine za Kiafrika. “Tanzania ni kito cha maendeleo ya Afrika.” Alisema.
Eton haikufundisha wanasiasa na viongozi tu bali pia wasanii, wanamichezo na wanasayansi. Mmojawapo ni mbunifu wa kisa mashuhuri cha James Bond , mwandishi Ian Fleming, aliyefariki mwaka 1964. Picha ya Fogs Movies Reviews.
Labels:
MICHEZO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment