Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Saturday, 21 December 2013

Wazaramo: Kabila lenye sherehe lukuki, usipochangia, kushiriki unatengwa



watoto wakipongezwa na wazazi baada ya kutoka jandoni katika mkoa wa pwani. Picha ya Maktaba
Na Aziza Nangwa, Mwananchi
Tanzania ni nchi iliyojaliwa kuwa na makabila zaidi ya 120, yaliyounganishwa na lugha moja ya taifa ambayo ni Kiswahili. Miongoni mwa makabila hayo ya Tanzania, limo Kabila la Wazaramo, ambalo linapatikana katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

Wazaramo wametapakaa katika Wilaya za Kisarawe, Bagamoyo, Kibaha, Mkuranga na Mafia. Jijini Dar es Salaam, wengi wanaishi katika maeneo ya Buguruni, Magomeni, Ilala, Kariakoo na Msasani.


Wengi wa Wazaramo wanaabudu katika madhehebu ya dini za Kiisalamu, Kikristo na madhehebu mengine kwa uchache.


Mbali na swala la dini, katika masuala ya chakula na mavazi, wengi wao hupendelea kula wali, ugali wa muhogo, sembe kidogo, chapati na maandazi.


Upande wa mavazi, wanawake wa Kizaramo hupendelea kuvaa zaidi magauni marefu na mitandio (madira), khanga mbili kwa kufunga moja kiunoni nyingine kujitanda hasa kwa wasichana ambao tayari wameshavunja ungo(wamebalehe).


Kabila hili linasifika kwa kupenda sherehe, ambapo katika makala haya Mwananchi Jumamosi lilifanikiwa kuzungumza na Mwajabu Akide ambaye ni ajuza, mkazi wa Kijiji cha Mengwa wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani anayeelezea mtiririko wa sherehe za Kabila la Wazaramo. Mwajabu anaelezea pia utamaduni, mila, desturi, sherehe za Wazaramo na maana yake, tangu mtoto anapozaliwa hadi anapokuwa na familia yake, naye kupata watoto wake.


Kwa mujibu wa Mwajabu, mtoto anapozaliwa katika familia ya Kizaramo, ndugu na jamaa wanapewa taarifa ambapo hutafutwa sheikh au mtu yeyote mwenye upeo katika dini ili kumfanyia adhana mtoto husika. Kitendo hiki hufanyika kama ishara ya kumkaribisha duniani na kumkumbusha wajibu wake kama binadamu mbele ya Mwenyezi Mungu na anachotakiwa kufanya katika maisha yake.


Anasema kuwa baada ya hapo mama na mtoto huendelea kukaa ndani kwa muda wa siku saba, kabla ya mtoto huyo kutolewa nje.


“Siku ya saba, mtoto huyo hutolewa nje huku kukiwa na ungo mdogo maarufu kwa jina la Kitunga na hapo mtoto anatolewa mara moja ili kuona upepo wa nje. Baada ya hapo hurudishwa ndani na mama yake mpaka siku ya arobaini,” anasema Mwajabu.

Sherehe ya kwanza

Mwajabu anabainisha kuwa, ikifika siku ya arobaini kwa wale wenye uwezo, huitisha sherehe ya Maulid ili mtoto anyolewe nywele za utoto na hapo dua ya kumshukuru Mungu kwa kumfikisha hatua hiyo husomwa, huku wengine wakiitisha ‘rusha roho’ kwa ajili ya kusherehekea siku hiyo baada ya Maulidi (Maulidi ni neno la Kiarabu lenye maana ya kuzaliwa).
Sherehe ya pili


Anaongeza kuwa, baada ya arobaini, mtoto wa Kizaramo akifikisha umri wa miaka miwili kwa wenye uwezo huwafanyia ‘Hakika’ au wengine huandaa sherehe ya kuzaliwa (birthday).


“Katika sherehe hii ya hakika huchinjwa mbuzi na kupikwa pamoja vyakula vingine. Pia hufanyika dua maalumu ya kumwombea mtoto,” anasema Mwajabu.


Sherehe ya tatu


Mwajabu anafafanua kwamba, mtoto akifikisha umri wa miaka mitatu na kuendelea, ikiwa ni wa kike huachwa, lakini wa kiume hupelekwa kupewa sunna (kutahiriwa).


Anaongeza kuwa, katika tukio la kutahiriwa kunakuwa na sherehe ya mkusanyiko wa watoto wa rika moja, ambao hufanyiwa sunna wakiwa porini.


“Lakini ndugu, jamaa na marafiki nao hujumuika na watoto katika sherehe huko porini. Kunakuwepo na ngoma za kiasili mbalimbali kama Vanga , Tokomile na Mdundiko na hapo wazazi hutunza pesa, huku watu wakila, kunywa na kufurahi,” anasema mwanamke huyo.


Sherehe ya nne


Mwajabu anaendelea kusimulia akisema kuwa, baada ya sunna na sherehe ya tatu, katika sherehe ya nne watoto huenda jandoni ambapo hukaa huko wakipewa mafunzo kwa siku kadhaa na baada ya kupona huitishwa sherehe nyingine ya kuwatoa jandoni wali hao.


Anaeleza kuwa katika sherehe hiyo kila mzazi huja na familia yake na kumchezea ngoma mtoto wao kwa kumtunza nguo, vitu mbalimbali na hapo watu hula na kunywa kwa furaha.


“Sherehe hiyo inamuimarisha mtoto wa kiume kujijua na kuwa na heshima kwa wazazi hasa mama na baba yake. Katika sherehe hiyo kunakuwepo na ngoma za kienyeji na rusha roho ili mradi watu wafurahi,” anasema na kuongeza:


“Ukiachilia mbali suala la watoto wa kiume, kwa watoto wa kike, akivunja ungo tu huwekwa ndani kwa muda wa siku saba na kuelekezwa mila na desturi kwa kufundishwa namna ya kujiweka msafi na kuwa na heshima,” anasema.


Anafafanua kuwa katika sherehe hiyo ndogo, mtoto wa kike hununuliwa nguo na kupikwa chakula kidogo siku ya kutoka ambapo watu wakasherehekea na kumpa maneno machache yaliyo mwongozo wa kujiheshimu na kujilinda.


Anasema: “Sherehe hii inamuimarisha mtoto aweze kujitambua akiwa katika siku zake na kuvaa nguo za heshima.”


Anaongeza kuwa, mafunzo hayo humjenga mtoto katika umri huo mbele ya watu hasa watu anao waheshimu na watoto wadogo na kutofanya mapenzi kabla ya kuelekezwa mila na desturi au kuolewa.


“Taratibu hizi zilikuwa zinawafanya watoto wa Kizaramo wasikutane na wanaume hadi waelekezwe mila na desturi au kuolewa, tena mila ya Kizaramo hawamchezi ngoma mtoto mwenye ujauzito,” anasema Mwajabu.


Anabainisha kuwa, baada ya hapo mtoto huendelea na shule hadi akimaliza masomo yake ndipo huwekwa ndani na huko anaweza kuwekwa kwa miezi au miaka kutegemea uwezo wa wazazi walivyojioanga kwa sherehe.


“Msichana akiwa ndani anajisugua kwa mapumba ya mahindi (chachu), bila ya kuoga. Hiyo inakuwa ndiyo maji yake ya kuoga, japo kuna wachache wanaoga, lakini wengine wanajisugua kwa mapumba bila ya kuoga na wanakuwa weupe wanang’aa na kuvutia watu,” anasema na kuongeza; “Baada ya kukaa miezi kadhaa au miaka, ndipo wana ndugu wanaitisha kikao na kujadiliana namna ya kugawana majukumu ya kufanya sherehe ikiwamo vifaa vya mwali, vyakula na ngoma.”


Anaongeza kuwa uamuzi wa kikao hicho unategemea wazazi wa mhusika wamejipanga vipi, kwani sherehe ya ngoma ina gharama kubwa.


“Suala la kupanga ngoma ya kumcheza mtoto hutegemea na mtoto na wazazi kwani, watoto wengi sasa wanasoma hivyo wazazi wengi hawapendi kuwaweka watoto siku nyingi ndani,” anasema.


“Sherehe za ngoma ya kumcheza mwali hupangwa ndani ya siku saba, lakini siku ambazo ngoma hupingwa na watu kula na kushereheka ni Jumatano hadi Jumapili hiyo ni kwa zamani, lakini sasa watu wengi hufanya sherehe kwa siku mbili kulingana na hali ya kipato cha wazazi husika,” anafafanua.


Anaendelea kusimulia kuwa, katika sherehe hii chakula kikuu huwa ni wali au pilau, hivyo kutokana na hali ya maisha na gharama zilivyopanda, wengi hufupisha siku za sherehe.


“Sherehe hiyo ya kucheza mwali huitwa Mkole ambapo mtoto wa kike hufunzwa vitu vingi vya kimaisha ikiwamo namna ya kuishi na watu wa jamii yake na baada ya hapo hutolewa nje akiwa amepambwa kama bi harusi,” anasema Mwajabu.


Anasema kuwa katika kumtoa mwali anaweza akatolewa kwa muziki, ngoma ya kienyeji au kwa Maulidi na hapo ndugu na jamaa hukusanyika na kumpa zawadi.


“Katika ugawaji wa zawadi hizo mtoto wa kike hupewa zawadi nyingi kuliko wa kiume. Hupewa zawadi ya nguo mbalimbali , kitanda , godoro vyombo vya nyumbani, vito vya dhahabu, meza za vyakula, mazuria, friji, jiko la umeme ,feni na vingine,” anasema Mwajabu.

No comments:

Post a Comment