Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Friday, 20 December 2013

Linah na Recho pete na kidole

Kawaida imezoeleka kwamba wasanii wanaofanya muziki wa aina moja huwa hawapatani na mara nyingi hushindwa kuwa karibu kutokana na kunyang’anyana mashabiki, kugombea shoo au ubize unaowafanya washindwe kukutana mara kwa mara.
Lakini kwa Estelina Sanga ‘Linah’ na Winfrida Josephat maarufu ‘Recho’ hali ni tofauti. Kwa nini? Hawa ni wasichana wanaofanya vizuri katika muziki wa kizazi kipya kwa sasa, lakini kuna kitu kilicho ndani yao ambacho kilikuwepo tangu miaka sita nyuma. Linah na Recho ni marafiki wanaopendana sana.

Wawili hawa ni watu wa makabila yasiyo na ukaribu kabisa. Linah ni msichana mwenye asili ya Makete kabila la Wakinga, huku Recho akitokea Kigoma kutoka katika kabila la Waha.
Walivyokutana


Miaka sita nyuma wasichana hawa walikuwa na matarajio ya kutimiza ndoto zao walizoziota kwa miaka kadhaa, huku wakijipa matumaini ya kufikia hatua hizo walizoamini kwamba ipo siku zitatimia.


Tangu wakiwa katika Nyumba ya Vipaji Tanzania, (Tanzania House of Talent-THT) mwaka 2009, walipata kuwa marafiki wakubwa ambao walikuwa wakifundishana mambo mbalimbali sambamba na kuchambua mbinu zilizoweza kuwaweka juu wasanii wakubwa wa kike kwa wakati huo, Mwasiti Almas na Vumilia enzi hizo wakiwachukulia kama nyota wao pale THT.


Enzi hizo Linah alikuwa ameibuka kidedea katika mchakato wa kumtafuta msanii anayejua kuimba, ambapo yeye na Ben Pol walifanikiwa kuibuka washindi na nyota hizo zinazong’aa mpaka sasa. Hicho ndiyo kilikuwa chanzo cha Linah kuonana na Recho pale THT alipokwenda kujifunza zaidi muziki.


Linah anasema “Nilikutana na Recho kabla sijawa staa enzi hizo nilikuwa kwenye matengenezo ya sauti yangu pale THT na tulikuwa tukisoma darasa moja, nilianza urafiki naye na kwa kipindi cha miezi kadhaa nilifanikiwa kutoa singo yangu ya kwanza ‘Atatamani’.”


Anasema kwa kipindi chote alichokaa na Recho hakuweza kumfahamu vizuri lakini aliendelea kumjua zaidi kwani hata alipofanikiwa aliendelea kumpenda japokuwa yeye mafanikio yake yalikuja baadaye sana.


“Recho namchukulia kama mdogo wangu kwani nilikaa naye darasani kwa kipindi kirefu tu na hata nilipotoa ‘Atatamani’ hakuweza kukaa mbali nami bali aliweza kunishauri vizuri mpaka nikafikia hatua ya juu zaidi, hata hivyo niliweza kumpa moyo kwamba anaweza na kumsaidia pale alipokwama kimuziki,” anasema.


Anafafanua kwamba anamchukulia Recho kama mdogo wake. “Damu zetu zimeendana sana na Recho huwezi kuamini sijawahi hata kugombana naye tofauti na rafiki wengi niliowahi kuwa nao, ukituona kama tupo mbali tambua majukumu ya kikazi yanatuweka mbali, lakini namchukulia kama mdogo wangu kwani ni zaidi ya rafiki,” anasema Linah.


Kwa upendo wake Recho anamwelezea Linah kama dada yake aliyemwezesha kwa kiasi kikubwa kufikia hatua ya juu aliyoifikia sasa.“Mimi na Linah tumekuwa marafiki tangu kitambo sana mimi sijatoka yeye hajatoka. Urafiki wetu umejengwa na mengi kwanza kabisa sisi tunatokea katika lebo moja yaani THT, hata baada ya kumaliza chuo cha muziki tumekuwa tukifanya kazi ofisi moja yeye ni rafiki yangu sana tu kwani tumezoeana kupita kiasi.

“Napenda kila kitu kutoka kwake na pia yeye ndiye mtu ninayejifunza kutoka kwake kila siku mpaka leo huwezi amini Linah ana vitu fulani ambavyo ni vizuri na mimi nimekuwa nikijifunza mambo mengi kutoka kwake kupitia kwanza tabia yake, uvumilivu alionao na juhudi katika kitu alichodhamiria kukifanya.”

Linah na Recho ameshawahi kuishi pamoja; “Awali tumeshawahi kuishi nyumba moja, ila baada ya mambo kuwa mengi tukaona ni vyema kila mmoja akatafuta makazi yake kwani tulikuwa tukifanya kazi kwa utofauti kwa kiasi kikubwa,” anasema Recho.


Linah amewahi kutamba na wimbo Atatamani, Fitina, Najua, Bora Nikimbie, Angalau Sasa, Ushafahamu, Lonely huku Recho alitamba na vibao kama Kizunguzungu, Mwali Kigego, Upepo na nyinginezo.

No comments:

Post a Comment