Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Friday, 20 December 2013

Extra Bongo; bendi inayoongoza kwa burudani ya ‘unenguaji’ nchini

Mashabiki waliowahi kuhudhuria maonyesho ya bendi ya muziki wa dansi nchini ya Extra Bongo watakubaliana nami kwamba ina wacheza shoo (madansa) makini, wenye uelewa mpana na pengine kukonga zaidi nyoyo za mashabiki katika tasnia hiyo.
Bendi hiyo iliyo chini ya Ally Choki maarufu Mzee wa Farasi, kikosi chake cha madansa kinaongozwa na Hassan Mohamed (Super Nyamwela) aliye na zaidi ya miaka 22 katika tasnia ya uchezaji wa dansi akiwa pia mkufunzi kwa kila dansa anayejiunga na bendi hiyo.

Meneja wa bendi hiyo Juma Kasesa anasema kazi anayoifanya Nyamwela ndiyo inayozidi kuipandisha chati bendi hiyo kila uchao na kwamba tangu Nyamwela alipojiunga na Extra Bongo kutoka Twanga Pepeta, idara hiyo ya shoo ndiyo inayoipaisha zaidi bendi yao.


“Bendi inazidi kuimarika kila siku na tumegundua kwamba madansa ndiyo wanaoinogesha zaidi wakichangiwa na vibao vikali vinavyotungwa na wanamuziki makini kama Ali Choki na kundi lake.


Tuna watunzi wazuri kwani kwa upande wa tungo tumeimarika. Tuna wanamuziki kama Athanas Muntanabe, rapa Frank Kabatano, Papii Katalogi aliyetokea Acudo, hao ni kati wasanii chachu ya bendi hii,” anasema Kasesa. Akizungumzia uhalisia wa bendi hiyo Kasesa anasema kuwa Extra Bongo ilianzishwa mwaka 2003 ikiwa na waimbaji Ally Choki, Bashiri Uhadi, Bob Kissa, Richard Maarifa, Khalidi Chokoraa, Flora Moses, rapa Greyson Semsekwa, (solo) Bonzo Kwembe, Efraim Joshua, George Gama (besi) Rythm na Thabit Abdul akipiga kinanda, huku drum zikipigwa na Imma Chokolate.


“Albamu ya kwanza iliitwa 3x3, wimbo uliokuwa kwenye albamu. Nyingine ni Regina Zanzibar, Tuchunge Wazazi au Fikiri Madinda, Nunu Milenium, Walimwengu Remix na Odise,”anaeleza.


Anasema kuwa tangu wakati huo bendi hiyo inatikisa anga ya muziki wa dansi nchini na kwamba ujio wa Extra Bongo uliongeza ushindani wa muziki wa dansi kwa bendi nyingine.


“Tuliendelea kujiimarisha kimuziki kwa kutoa albamu ya pili iliyoitwa ‘Bullet Proof’ ikiwa na nyimbo kama Double Double, lakini safari hii ikiwa chini ya mpiga drum mpya James Kibosho. Ilikuwa na nyimbo nyingine kama Richi Maarifa na Lengo halijatimia, ukiwa ni utunzi wa Thabit Abdul, Namaliza kwa shingo Upande, Nitamlilia nani na Papa Msofe, zilitungwa na Ally Choki, anabainisha Kasesa na kuongeza:


“Kama ilivyo msemo wa Kiswahili; Ngoma ikivuma sana hupasuka, hatimaye mwaka 2004 Extra Bongo ilisambaratika baada ya baadhi ya wanamuziki kuchukuliwa na Asha Baraka kwenda kuasisi bendi yake mpya ya Madikodiko wakiwamo Khalid Chokoraa na Thabit Abdul na huo ukawa mwisho wa awamu ya pili ya bendi.”


Anaeleza kuwa baada ya kusambaratika kwa bendi hiyo, Choki aliungana na Muumini Mwinjuma ambapo waliunda Bendi ya Double Extra ikiwa ni muunganiko wa Extra Bongo na Double M iliyokuwa chini ya Muumin. Extra Bongo ilifufuliwa tena mwaka 2009 na hadi leo ikiwa inaendelea kutamba ambapo albamu ya kwanza kutoka iliitwa Mjini Mipango, ambapo sasa wana albamu nyingine inayotamba kwa jina la Ufisadi wa Mapenzi.


Kasesa anawataja baadhi ya wanamuziki waliopo Extra Bongo kuwa ni pamoja na Adamu Bombole, Redo Maugo, Athanas Muntanabe, Richard Maarifa sanjari na wapiga vyombo Said, Adamu Hassan, Sam Kibosho na Chakuku Tumba akiongeza kumtaja Khadija Mnoge mwimbaji wa kike wa bendi hiyo.


Aliweka wazi kwamba wanamuziki wawili wa bendi hiyo walisimamishwa kazi kutokana na utovu wa nidhamu na kwamba sasa wanatarajiwa kuonekana tena mwishoni mwa mwaka huu.


Anaeleza kuwa kuna changamoto nyingi zinazoikabili bendi hiyo kwa sasa ikiwemo nyimbo zake kutopewa muda wa hewani katika vituo vya redio na televisheni hata kazi nyingine za muziki wa dansi nchini.
“Changamoto kubwa ni kwa vyombo vya habari hasa redio na televisheni kuacha kupiga muziki wa dansi, inatuumiza sana bendi nyingi za muziki wa dansi, sasa hivi hazipigi muziki wetu, muziki wetu umefifia sana kutokana na mashabiki wengi kutopata nafasi kubwa kutuona jukwaani, hawajui tunafanya nini na tumetoa wimbo gani,” analalamika Kasesa.

No comments:

Post a Comment