Wednesday, 9 October 2013
IFAHAMU DAMU YA KIARABU,YENYE URAIA WA UJERUMANI,ILIYOKULIA HISPANIA NA KWENDA LONDON
Kiungo wa Arsenal,Mesut Ozil
NYOTA aliyesajiliwa kwa gharama kubwa msimu huu katika kikosi cha Arsenal ni Mesut Ozil. Nyota huyu tayari amethibitisha ubora wake kwa kuonyesha uwezo wa kujitambua, kutuliza na kutoa pasi sahihi, pia ana uwezo wa kucheza kitimu.
Ozil ambaye ni raia wa Ujerumani mwenye asili ya Uturuki alisajiliwa na Arsenal msimu huu kwa Pauni 42.5 milioni akitokea klabu ya Real Madrid na kusaini mkataba wa kuitumikia Arsenal kwa miaka mitano.
Baada ya kusaini mkataba huo, Ozil alipohojiwa na vyombo vya habari alisema: “Ni kweli nilitaka kubaki Real Madrid, lakini baadaye niligundua kwamba kocha au benchi la ufundi halina imani na mimi. Mimi ni mchezaji ninayependa kuaminika, ndiyo maana nimehama Madrid na kujiunga na Arsenal ambayo inaonyesha itaniamini.”
Hata hivyo, wachezaji wengi wa Real Madrid hawakufurahishwa na uamuzi wa Ozil kuhama Real Madrid, miongoni mwao alikuwa ni nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo ambaye alisema: “Alikuwa ni mchezaji anayejua kwa kiwango cha juu kunichezesha tukiwa tunashambulia, nimekasirika kwa kuondoka Ozil.”
Kutuliza na kutoa pasi sahihi
Ozil aliichezea Arsenal kwa mara ya kwanza Septemba 14, 2013 katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Sunderland ugenini, katika mechi hiyo alimpa pasi nzuri Olivier Giroud aliyeitumia vizuri kuipatia Arsenal bao dakika ya 11. Mechi hiyo ilimalizika kwa Arsenal kushinda 3-1 ikiwa ni mechi ya nne msimu huu wa ligi.
Siku tatu baadaye, Ozil aliichezea Arsenal kwa mara ya kwanza katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Marseille, ambapo Arsenal iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 ugenini ambayo yalifungwa na Theo Walcott na Aaron Ramsey.
Ozil aliichezea Arsenal mechi yake ya kwanza ikiwa nyumbani wakati walipocheza na Stoke City Septemba 22 na Arsenal kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 huku mabao ya Arsenal yakifungwa na Aaron Ramsey, Per Mertesacker na Bacary Sagna.
Pia Septemba 28, Arsenal ilicheza dhidi ya Swansea na kushinda 2-1 hivyo kukaa kileleni mwa Ligi Kuu England.
Katika mechi zote hizo Ozil alifanya vizuri katika kutuliza mpira na kutoa pasi sahihi.
Oktoba 2, Ozil alidhihirisha ubora wake baada ya kuiongoza Arsenal kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Napoli katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Katika mechi hiyo alifunga bao la kwanza katika dakika ya nane na baadaye alitoa pasi kwa Olivier Giroud aliyeipatia Arsenal bao la pili katika dakika ya 15.
Si mbinafs
Ozil ni kiungo mshambuliaji anayejionyesha kwa jinsi anavyocheza, haijifichi, ana kipaji cha juu ingawa ni hatari kuwa na mchezaji maarufu katika sehemu inayohitaji ubunifu ambayo ni kiungo mshambuliaji au mchezeshaji wa timu. Kama mchezaji anayecheza sehemu hiyo ya kiungo ni mbinafsi, basi atashindwa kutekeleza wajibu wake wa kuiendesha timu. Lakini Ozil yupo tofauti, yeye anacheza kitimu zaidi, ana uwezo wa kuwadanganya wachezaji wa timu pinzani na hivyo kuwapa nafasi washambuliaji kuwa huru na kuwapasia wakiwa katika sehemu nzuri ya kufunga. Ozil alifanya hivyo alipokuwa Real Madrid, alikuwa akimpa pasi nzuri za kufunga Cristiano Ronaldo na anafanya hivyo kwa Giroud katika Arsenal.
“Wachezaji wenzangu wananijua mimi ni mchezaji ambaye si mbinafsi,” alisema Ozil alipojiunga na Arsenal.
Fundi wa mipira ya adhabu
Ozil ni fundi wa kupiga mipira ya adhabu. Anatarajiwa ataisaidia sana Arsenal katika kupiga mipira ya adhabu ambayo italeta mabao. Katika mechi ya Ligi Kuu waliyocheza dhidi ya Stoke City Septemba 22 na Arsenal kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, mabao yote ya Arsenal yalipatikana kutokana na mipira ya adhabu iliyopigwa na Ozil.
Mchezaji asiyetumia nguvu nyingi
Upo msemo usemao kuwa mashabiki wa soka wa England wanapenda kuona wachezaji wanaojituma, wanaotumia nguvu, wachezaji wanaokimbiza mpira muda wote uwanjani, lakini katika miaka ya hivi karibuni wameibuka pia mashabiki wanaopenda wachezaji wanaocheza taratibu bila kutumia nguvu nyingi, wanajituma na kutumia akili nyingi uwanjani kama Dimitar Berbatov. Uchezaji huo wa taratibu bila kutumia nguvu nyingi, kujituma na kutumia akili nyingi uwanjani, mwenyewe ni Mesut Ozil.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment