Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Monday 21 October 2013

SIMBA YANYWA MAJI JANGWANI,NI BAADA YA KUCHOMOA GOLI TATU.


Mashabiki wa Simba wakishangilia katika mchezo wa watani wa jadi dhidi ya Yanga
uwanja wa taifa jiji Dar er Salaaam na kutoka sare ya magoli 3-3.

HII haijawahi kutokea! Kwa mechi ya watani wa jadi inaweza kuwa historia. Dakika 45 za mwanzo ungedhani Mnyama amechinjwa, lakini huwezi kuamini kwani Simba walisema: “Hawatuwezi.”
Yanga iliyocheza kwa mbwembwe dakika 45 za mwanzo iliondoka na kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo ikiwa inaongoza kwa mabao 3-0, lakini hali ilibadilika kipindi cha pili baada ya Simba aliyejeruhiwa kuingia kwa kasi uwanjani na kusawazisha mabao yote matatu na kuufanya ubao wa matokeo usomeke 3-3 mpaka dakika ya mwisho ya mchezo.
Kwa matokeo hayo, mashabiki wa Simba wanaona kama wameshinda mchezo, kwani wanaamini kusawazisha mabao hayo ni ushujaa mkubwa na hakika wanastahili kujisifu kwa hilo.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana Jumapili, Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 14 mfungaji akiwa, Mrisho Ngassa.
Ngassa alifunga bao hilo kutokana na juhudi za Mrundi, Didier Kavumbagu aliyeambaa vizuri na mpira na kumpasia Hamis Kiiza ambaye alimuunganishia Ngassa aliyeujaza wavuni akiwa katikati ya mabeki wawili wa Simba, Gilbert Kaze na Joseph Owino.
Kiiza afanya kweli
Yanga waliongeza bao la pili dakika ya 35 mfungaji akiwa ni Kiiza. Mpira ulirushwa na Mbuyu Twite na Kavumbagu akaupiga kichwa kwa nyuma na kumkuta Kiiza aliyeujaza wavuni.
Awali kipa wa Simba Abel Dhaira alitaka kuufuata mpira uliorushwa na Twite lakini akasita na ndipo Kavumbagu alipotumia nafasi hiyo kuupiga kichwa na Kiiza kuujaza wavuni kwa shuti la mguu wa kulia.
Yanga iliandika bao la tatu dakika ya 45 mfungaji akiwa ni Kiiza tena. Kiiza alifunga bao hilo kutokana na mpira ulioanzia kwa Haruna Niyonzima ambaye aliukokota vyema na kumuunganishia Kavumbagu.
Kavumbagu licha ya kuonekana yuko katika nafasi nzuri ya kufunga, hakuonyesha ubinafsi, alimuunganishia pande safi Kiiza aliyeujaza wavuni.
Mashabiki Simba wasusa
Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa mabao yao matatu hali iliyowafanya baadhi ya mashabiki wa Simba kuanza kuondoka uwanjani na kufanya baadhi ya majukwaa ya upande wa Simba kuwa tupu
Wakiwa katika hali ya huzuni mashabiki hao walionekana wakiinuka vitini mmoja mmoja wakiamini kwamba timu yao ingefungwa mabao mengi zaidi.
Hatua hiyo ya mashabiki hao pengine ilichangiwa na kucheza hovyo kwa timu hiyo na kuruhusu mabao ambayo yalitoa dalili ya mvua kuwa wangefungwa zaidi kipindi cha pili.
Lakini ikawa si hivyo kwani Simba iliingia kipindi cha pili na nguvu mpya baada ya kupewa maelekezo na kocha wao, Abdallah Kibadeni ‘Mputa’ ambaye pia aliwatoa, Abdulhalim Humoud ‘Gaucho’ na Haruni Chanongo wakaingia, Said Ndemla na William Lucian ‘Gallas’ dakika ya 46.
Vijana wa maajabu
Kuingia kwa Ndemla na Gallas ambao wamepandishwa kutoka timu ya vijana kuliifanya Simba ing’are kwani safu ya kiungo ilitawala zaidi na kuifanya safu ya ushambuliaji, iliyokuwa imesinzia kipindi cha kwanza kuamka na ikawa urahisi kwa Betram Mwombeki na Mrundi Amis Tambwe kupata mipira mingi na dakika ya 53 Mwombeki aliwafungia Simba bao la kwanza.
Mwombeki alifunga bao hilo akiwa yeye na kipa wa Yanga, Ally Mustaph ‘Barthez’ baada ya mabeki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani kujichanganya na wote kumkaba Amis Tambwe.
Wakati mabeki hao wakipambana na Tambwe, mchezaji huyo kutoka Burundi alimsogezea mpira Mwombeki ambaye aliujaza wavuni kiulaini.
Simba wazidi kucharuka
Dakika tatu baada ya bao hilo, kasi ya Simba iliongezeka na kulisakama lango la Yanga ambao mabeki wake na safu ya kiungo walionekana kama wamechanganywa na kasi hiyo ya vijana wa Msimbazi.
Hatimaye mpira wa kona uliopigwa na Ramadhan Singano ‘Messi’ dakika ya 56 uliwapita wachezaji wa Yanga na kumkuta Joseph Owino ambaye aliujaza wavuni kwa kichwa na mpira kumshinda kipa wa Yanga, Ali Mustapha ‘Barthez’ ambaye licha ya kuurukia lakini akawa kama anausukumizia wavuni.
Mabao hayo yaliamsha ari zaidi na kufufua matumaini ya wachezaji wa Simba na kwa mara nyingine juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 83 kwa bao la Gilbert Kaze aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Nassor Said Chollo.
Bao hilo lilizidi kuwaweka mashabiki wa Yanga katika wakati mgumu wasiamini kilichokuwa kikiendelea uwanjani huku wale wa Simba wakionekana kupagawa kwa furaha.
Kabla ya Simba kufunga bao la tatu, dakika ya 64, Ngassa aliichambua safu ya ulinzi ya Simba na kufumua shuti kali akiwa karibu na kipa Dhaira lakini kipa huyo alionyesha umahiri wake kwa kuruka na kudaka shuti la Ngassa la kimo cha mbuzi ambalo lilielekezwa upande wa kushoto wa kipa huyo.
Simba nayo ilikuja juu dakika ya 72 baada ya Jonas Mkude kuufumania mpira nje ya eneo la 18 na kufumua shuti ambalo lilipaa juu ya lango la Yanga.
Kipindi cha kwanza kilikuwa kigumu mno kwa Simba ambao walionekana kujichanganya kiasi cha kuruhusu mabao hayo matatu huku wakishindwa kulitia misukosuko lango la Yanga.
Baada ya mechi hiyo, nahodha wa Simba, Chollo alisema kuwa Yanga walicheza vizuri kipindi cha kwanza na wao walifanya hivyo kipindi cha pili:
“Kipindi cha pili tulipewa maelekezo na makocha wetu tukayafuata, tunashukuru tumeweza kusawazisha na tulikuwa tunatafuta bao la kuongeza lakini muda haukuruhusu.
Simba: Abel Dhaira, Nassor Cholo, Haruna Shamte, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhan Singano, Abdulhalim Humoud/William Lucian, Betram Mwombeki/Zahor Pazi, Amis Tambwe na Haroun Chanongo/Said Ndemla.
Yanga: Ali Mustapha Barthez, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Cannavaro, Kelvin Yondani, Athuman Idd Chuji, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngassa na Hamis Kiiza/Simon Msuva.
Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 19 katika mechi zake tisa wakati Yanga ambayo pia imecheza mechi tisa imefikisha pointi 16. Matokeo hayo yanafafanishwa na fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2005 wakati Liverpool walipotoka nyuma ya mabao matatu na kusawazisha yote mpaka kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

No comments:

Post a Comment