Monday, 21 October 2013
KASEJA AWEKA REKODI NYINGINE,AANGALIA MECHI YA WATANI WA JADI JUKWAA KWA MARA YA KWANZA
Alikuwa kipa wa Simba Juma Kaseja
KWA mara ya kwanza baada ya miaka kumi kipa namba moja wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Juma Kaseja, anakosa hata kuwapo kwenye benchi la akiba pale watani hao watakapovaana Jumapili.
Kaseja atakuwa ameketi katika mojawapo ya viti vya jukwaani akiwa mshangiliaji baada ya kuweka historia hiyo ya miaka 10 kuwa langoni, ambapo kwa miaka tisa alikuwa akiidakia Simba na mmoja alikuwa Yanga.
Kama Kaseja atakuja uwanjani uwezekano mkubwa ni kwa kipa huyo kuingia uwanjani kama shabiki mwingine na kukaa jukwaani akiziangalia timu hizo zikipambana.
Kwa sasa Kaseja hana timu, zaidi yupo mtaani na wakati mwingine anafanya mazoezi yake binafsi baada ya kushindwa kupata timu ya kuchezea msimu huu.
Mara baada ya kumaliza mkataba wake na Simba, kipa huyo alikuwa akihusishwa na mipango ya kujiunga na FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mpango ambao hata hivyo haukufanikiwa.
Klabu nyingine ambazo zilihusishwa na mipango ya kumsajili kipa huyo mahiri ni za hapa Bongo ambazo ni Lipuli ya Iringa (Ligi Daraja la Kwanza), Ashanti United, Mtibwa Sugar na Coastal Union (zote za Ligi Kuu Tanzania Bara).
Mchezo wa kwanza wa watani ambao Kaseja alicheza ulikuwa Aprili 20, 2003 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza akiidakia Simba. Yanga ilishinda mabao 3-0, wafungaji wakiwa Kudra Omary (dk ya 30), Heri Morris (dk ya 32) na Salum Athumani (dk ya 47).
Mchezo wake wa mwisho wa watani ulikuwa Mei 18 mwaka huu pia akiidakia Simba ambayo ililala mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, mabao yalifungwa na Mrundi Didier Kavumbangu na Hamisi Kiiza dakika ya 5 na 62.
Hii ni rekodi ya michezo 25 ambayo Kaseja aliidakia Simba dhidi ya Yanga.
Mwaka 2003
Mchezo wa kwanza ulikuwa wa kirafiki Aprili 20, 2003 katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. Yanga ilishinda mabao 3-0.
Kisha zikaumana katika Ligi Kuu, Septemba 28 na matokeo yalikuwa sare ya 2-2. Mchezo wa tatu mwaka huo ulikuwa wa marudiano Ligi Kuu Novemba 2 na matokeo kuwa suluhu.
Agosti 7, 2004 ulichezwa mchezo wa nne ambapo Simba ilishinda mabao 2-1 wakati kwenye mchezo mwingine Septemba 18, Simba ilishinda 1-0.
Mwaka 2005
Aprili 17, 2005 alicheza mchezo wa sita, Simba ikashinda tena 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro. Wakakutana tena Julai 2 kwenye fainali ya Kombe la Tusker Kirumba, Mwanza na Yanga ikalala 2-0.
Agosti 21, Simba iliishinda Yanga 2-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Mwaka 2006
Machi 26, 2006, Simba na Yanga zilitoka sare ya bila kufungana kwenye Ligi Kuu wakati Agosti 15, kwenye mchezo wa kumi wa Kaseja matokeo yalikuwa sare ya 1-1. Lakini baadaye Simba ikashinda kwa penalti 7-6.
Mechi hiyo ilikuwa ya nusu fainali ya Kombe la Tusker. Mchezo wa 11 ulikuja Oktoba 29 wa Ligi Kuu ambao ulimalizika kwa sare ya bila kufungana.
Mwaka 2007
Mchezo wake wa 12 ulikuwa Julai 8 kwenye fainali ya Ligi Ndogo, matokeo yalikuwa 1-1 ndani ya dakika 120, lakini Simba ilishinda kwa mikwaju ya penalti 4-3. Ilikuwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro. Kwenye mchezo wa ligi kuu uliochezwa pia uwanjani hapo Oktoba 24, Simba ilishinda 1-0.
Mwaka 2008 (akiwa Yanga)
Mchezo wa 14 ulikuwa Aprili 27, 2008, hii ilikuwa mechi ya Ligi Kuu iliyoisha kwa sare ya 0-
Oktoba 31, ulikuwa mchezo wa 15 kwa Kaseja akiwa tayari amerejea Simba akitokea Yanga baada ya kumaliza mkataba wake wa mwaka mmoja na kuiongoza timu yake kipenzi kuilaza Yanga 1-0.
Mechi ya 16, ilikuja Desemba 25, mwaka huo kwenye nusu fainali ya Kombe la Tusker na Yanga ilishinda 2-1.
Mwaka 2010
Mechi ya 17 kwa nahodha huyo, ilikuwa mechi ya Ligi Kuu ya Aprili 18 ambapo Yanga ilichapwa mabao 4-3. Oktoba 16 pia kwenye Ligi Kuu, Yanga ilishinda 1-0. Ziliumana Uwanja Kirumba, Mwanza.
Mwaka 2011
Mechi ya 19 ilikuwa Machi 5, timu hizo zilitoka sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa.
Mwaka 2012
Mechi ya 20 ilipigwa Julai 10, mwaka 2012, Yanga ilishinda 1-0, kwenye fainali Kombe la Kagame, wakati mechi ya 21 ilikuwa Agosti 17 ambapo Simba ilishinda 2-0 huku mchezo wa 22 uliochezwa Oktoba 29 Yanga ilishinda 1-0.
Mchezo wa 23 ni ule wa kufunga ligi msimu wa 2011/2012 na Yanga ilifungwa 5-0, mechi ambayo Kaseja aliifunga Yanga ndani ya dakika 90 kwa mkwaju wa penalti.
Mchezo wake wa 24 ulikuwa Oktoba 3 ambapo timu hizo zikitoka sare ya 1-1 katika Ligi Kuu.
Mwaka 2013
Mechi ya 25 na ya mwisho kwa Kaseja kuidakia Simba dhidi ya Yanga ilikuwa Mei 18 ambapo Simba ililala 2-0, huo ulikuwa mchezo wa mwisho wa ligi msimu uliopita.
Ikumbukwe kuwa msimu wa 2008/09, Kaseja alikwenda kuichezea Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja na huko aliwadakia mechi moja dhidi ya Simba, Aprili 19, 2009 na timu hizo kutoka sare ya 2-2. Mabao ya Simba yalifungwa na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ dakika ya 23 na Haruna Moshi ‘Boban’ dakika ya 62, wakati ya Yanga yalifungwa na Ben Mwalala dakika ya 48 na Jerry Tegete dakika ya 90.
Hadi anaachwa Simba, Kaseja ameiwezesha timu hiyo kutwaa mataji saba, matano ya Ligi Kuu Tanzania Bara katika misimu ya 2003, 2004, 2007 (Ligi Ndogo), 2010 na 2012 na mawili ya Tusker, mwaka 2003 na 2005 kwa mashindano yaliyofanyika Tanzania kisha Kenya.
Rekodi zake alipoichezea
Simba dhidi ya Yanga
Alicheza jumla ya michezo 25
Simba ilishinda michezo: 11
Simba ilipoteza michezo: 7
Sare michezo: 7
Wafungaji Bora kwa miaka 10 kwenye michezo kati ya Simba na Yanga
5. Emmanuel Gabriel (Simba)
Mussa Mgosi (Simba)
4. Jerry Tegete (Yanga)
Nico Nyagawa (Simba)
3. Haruna Moshi ‘Boban’ (Simba)
2. Amri Kiemba (Yanga/ Simba)
Athumani Machupa (Simba)
Credo Mwaipopo (Yanga)
Emmanuel Okwi (Simba)
Heri Moris (Yanga)
Hillary Echesa (Simba)
Kudra Omary (Yanga)
Staa wa Yanga wa sasa anayeongoza kwa kumfunga Kaseja ni Jerry Tegete (mabao manne)
Staa wa Yanga aliyeshindwa kumfunga Kaseja tangu aanze kuichezea Yanga ni Mrisho Ngassa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment