Na Mahmoud Zubeiry, Muscat
WACHEZAJI watatu wa timu ya soka ya Coastal Union ya Tanga, beki Juma Nyosso, kiungo Jerry Santo na mshambuliaji Danny Lyanga wanatakiwa na klabu ya Al Musannaa ya Ligi Kuu ya Oman, imefahamika.
Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata mjini hapa zimesema kwamba klabu hiyo imekwishakutana na
Jerry Santo kulia akiwa na Salum Esry jana kabla ya chakula cha usikuMwenyekiti wa Coastal Union, Hemed Hilal ‘Aurora’ kwa mazungumzo juu ya nyota hao.
Hata hivyo, habari zaidi zinasema makubaliano hayajafikiwa kutokana na Coastal kusema Musannaa imetoa ofa ndogo ya kuwanunua nyota wake hao. Inaelezwa, kiungo Mkenya, Jerry Santo anatakiwa pia klabu ya Fanja, ambayo hadi sasa ina mgeni mmoja tu kikosini mwake, Cisse wa Senegal.
Jana tena Aurora alikuwa ana kikao na uongozi wa Musannaa hata akashindwa kuhudhuria mwaliko wa chakula cha usiku, ambao Coastal walipewa na mwanachama wa timu hiyo anayeishi hapa, Salum Esry.
Aurora hakuwa wazi sana alipoulizwa leo asubuhi kuhusu maendeleo ya mazungumzo hayo, lakini Ofisa Habari wa Coastal, Hafidh Kido alisema dili hilo bao halijaiva.
Kuna uwezekano Musannaa ikaongeza dau kama itakuwa ina nia haswa ya kuwachukua wachezaji hao, kwa sababu Serikali ya Oman imetoa fedha zenye ya Sh. Bilioni 1 kwa kila klabu hapa ili zijiendeleze.
Klabu kama Fanja imetumia sehemu ya fedha hizo kwa kukarabati Uwanja wake wa mazoezi uwe Uwanja kamili wa kuutumia hadi kwa mashindano, wakati nyingine zinatumia kusajili na mipango mingine ya maendeleo.
Coastal inatarajiwa kucheza mechi yake ya nne katika ziara yake ya wiki mbili hapa tangu ifike Januari 9, kwa kumenyana na Seeb jioni ya leo.
Awali, Coastal ilizifunga 2-0 kila timu, Nadi Oman na Musannaa kabla ya kufungwa 1-0 na Fanja juzi na baada ya leo watacheza pia na Al Thuwaiq.
www.tabasamuleo.blogspot.com
No comments:
Post a Comment