Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Saturday 14 December 2013

MR. BEAN MCHEKESHAJI MWENYE ELIMU KUBWA KICHWANI

beenclip_ad596.jpg
KWENYE safari yake ya kwenda mapumziko nchini Kenya mwaka 2001, rubani wa ndege yake binafsi alizimia wakiwa angani na hapo akalazimika kuongoza ndege hiyo kwa dakika kadhaa kabla ya rubani huyo kuzinduka na kuendelea na safari.
Hii si kama ilikuwa sehemu ya vipande vya filamu zake za vichekesho, bali lilikuwa tukio halisi. Hapa anazungumziwa Mr. Bean, mchekeshaji mashuhuri duniani katika filamu za komedi.
Mr. Bean ambaye jina lake halisi ni Rowan Sebastian Atkinson, ni mwigizaji mashuhuri Mwingereza ambaye amepata umaarufu mkubwa duniani kutokana na kuigiza filamu za komedi.
Akiwa amezaliwa Januari 6, 1955 na kushiriki kwenye filamu mbalimbali ikiwamo za ucheshi za Mr. Bean na Blackadder, Atkinson amekuwa tajiri mkubwa miongoni mwa waigizaji wa komedi na kuwa na pato linalokadiriwa kuwa la Dola 130 milioni. Umahiri wa filamu zake za komedi ndizo zinazofanya ziendelee kupendwa hadi sasa na hivyo kumwingizia pesa
Jinsi alivyopiga pesa
Atkinson kwanza amepata sifa moja, kuwa mwigizaji maarufu zaidi Uingereza kutokana na kuigiza komedi. Alianza kuigiza kwenye redio kabla ya kuhamia kwenye televisheni na kisha kutengeneza mfululizo wa filamu za vichekesho zinazofahamika kama Mr. Bean.
Kufanikiwa kwa mfululizo huo na ile filamu yake ya Johnny English kulimfanya kuwa maarufu zaidi na kupanua wigo wa kipato chake cha pesa ambapo hadi kufika sasa, Atkinson anatajwa kuwa moja ya waigizaji wa komedi matajiri zaidi duniani.
Ameingiza pesa nyingi kutokana na kuigiza kwake kuanzia kwenye redio, televisheni hadi kwenye filamu. Alivuna Pauni 11 milioni kama ada ya ushiriki kwenye mfululizo wa filamu za Mr. Bean.
Dola 2 milioni nyingine aliziingiza baada ya kushiriki kwenye 'Blackadder' na kiasi kama hicho tena alikiingiza kwa kutokea kwenye matangazo mbalimbali ya benki.
Amewekeza pia kwenye kampuni ya upangaji wa vipindi vya televisheni na hivyo kumwongezea zaidi utajiri wake na kumfanya afikie kadirio hilo la kuwa na kipato cha Dola 130 milioni.
Umahiri wake kwenye kuigiza unaendelea kumwingizia kipato hadi sasa kutokana na kupata dili mbalimbali za matangazo licha ya kwamba mfululizo wa filamu zake za Mr. Bean umeripotiwa kufikia kikomo mwaka 2012.
Maisha ya starehe
Kutokana na kuwa na pesa za maana, Atkinson hataki kujibanabana na amekuwa akiishi maisha ya starehe nyingi ili kufurahia matunda yanayotokana na sanaa yake.
Anamiliki majumba ya kifahari sehemu mbalimbali ikiwamo Chelsea, London na Oxford zote zikiwa England. Ukiweka kando majumba yenye hadhi kubwa, Atkinson anamiliki pia magari mengi ya kifahari na yenye thamani kubwa.
Kwenye orodha ya magari hayo, kuna Audi R8, Honda NSX, Honda Civic Hybrid na McLaren F1 yenye uwezo wa kukimbia kwa kilomita 350 kwa saa.
Mr. Bean ni kichaa wa magari na mara kadhaa alipata ajali, lakini hakuwa amepata majeraha makubwa. Mwigizaji huyo pia anamiliki ndege yake binafsi Cessna 202. Pesa zake pia amekuwa akizitumia katika huduma mbalimbali za kijamii akijitolea kuchangia miradi ya UNICEF, Comic Relief, CAFOD & Save the Children.
Maisha binafsi na ndoa
Maisha ya Mr. Bean yamekuwa safi kabisa na hana shida. Alizaliwa na wazazi Waingereza akiwa mtoto wa mwisho kwenye familia ya watoto wanne. Ni mwigizaji ambaye elimu imelala kichwani kutokana na kuwa na Shahada ya Pili ya masuala ya umeme aliyoisomea kwenye Chuo Kikuu cha Oxford.
Kwenye maisha ya ndoa, alianza kujihusisha kimahusiano na mrembo mwenye asili ya India, Sunetra Sastry mwishoni mwa miaka ya themanini na mwaka 1990 alifunga naye pingu za maisha.
Wanandoa hao ambao wanatajwa kuwa kwenye mapenzi motomoto wamefanikiwa kupata watoto wawili.

No comments:

Post a Comment