Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Monday 9 December 2013

Kenya yaanza njama kwa Kili Stars

Mombasa.Wenyeji Kenya wameingia mchecheto na makali ya Kilimanjaro Stars baada ya kulazimisha mchezo wa nusu fainali ufanyike Machakos badala ya Mombasa.
Awali nusu fainali hiyo ilikuwa ichezwe Mombasa, lakini kutokana na hali ya joto ambayo inaibeba Tanzania kulinganisha na Kenya ambayo wachezaji wake wengi wanaishi Nairobi kwenye baridi.


Baada ya mechi dhidi ya Rwanda, ambapo Kenya ilishinda bao 1-0, Kocha Adel Amrouche alikiri kwamba; “Hali ya hewa ya Mombasa si nzuri kwetu ni joto kiasi na wachezaji wangu hawajazoea.”


Habari za ndani zinadai baada ya Uwanja wa Kisumu kushindikana kumalizika kwa wakati waandaji walipanga mechi za nusu fainali zichezwe Mombasa na fainali ikachezwe Nyayo mjini Nairobi, lakini kwa hali waliyoiona katika mechi za juzi Jumamosi wenyeji wakaamua kupeleka mechi ya Kili Stars dhidi ya Kenya huko Machakos. Mechi nyingine ya nusu fainali itachezwa mjini Mombasa.


Habari za ndani zinadai kwamba Adel amewaambia viongozi wake kwamba endapo Kenya ikicheza na Stars mjini Mombasa itakuwa kwenye wakati mgumu kutokana na Tanzania kuzoea hali ya joto na vilevile ina sapoti kubwa Mombasa kwa vile ni jirani na Tanga.


Kenya iko kwenye presha ya kufuzu fainali kwani siku ya fainali nchi hiyo itakuwa ikisherehekea miaka 50 ya uhuru wake.


UGANDA WAUTEMA UBINGWA


Uganda imeliachia Kombe la Chalenji baada ya kuchapwa kwa penalti 3-2 na Kilimanjaro Stars kwenye Uwanja wa Manispaa ya Mombasa.


Kocha wa Uganda, Sredejovic Milutin ‘Micho’ na wachezaji wake waliingia kwenye mchezo huo kwa kujiamini, ambapo walicheza kwa kutulia na kushambulia kwa kumtumia winga Dan Sserunkuma aliyetumia dakika 16 tu kufunga bao la kuongoza kabla ya Mrisho Ngassa kusawazisha dakika mbili baadaye na akafunga tena la pili dakika ya 38.


Beki mrefu wa Uganda, Martin Mpunga alifunga bao la pili la Uganda dakika ya 73 na kusababisha timu hizo kwenda kwenye penalti kwani dakika 90 zilimalizika kwa sare ya mabao 2-2.


Stars ilianza kuwachanganya Uganda mapema baada ya kusawazisha bao lao na kuwaongeza jingine na kuwalazimisha kwenda kipindi cha kwanza wakiwa nyuma kwa mabao 2-1.


Hali hiyo ilizua utata kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwani kocha Micho alisikika akiwafokea wachezaji wake na kuwaambia waache upuuzi kwa vile wamebeba hadhi ya mamilioni ya raia wa Uganda
Kipa Benjamin Ochan ndiye aliyekuwa kwenye wakati mgumu zaidi kwani wachezaji walikuwa wakimlaumu kwa mabao ya aina moja aliyofungwa na Ngassa.
Wachezaji hao waliingia uwanjani kipindi cha pili wakitaka kufunga bao la mapema, lakini ukuta wa Stars haukuruhusu hilo, jambo ambalo lilizidi kuwachanganya washambuliaji Emmanuel Okwi, Danny Serunkuma na Hamis Kiiza.
Micho alijivuna kwamba alikuwa akiingia kwenye mchezo huo akiwa na nafasi kubwa ya kushinda kwa madai kwamba ametengeneza wachezaji wengi wanaotumika kwenye nchi za Afrika Mashariki na Kati hivyo hana wasiwasi.
Lakini baada ya kutolewa alisema; “Tumekuja na kikosi kichanga ambacho lengo letu kubwa lilikuwa kutengeneza timu imara ya CHAN, ingawa pia tulitaka kutetea ubingwa wetu.”


“Tanzania ni ngumu, lakini inapofika kwenye suala la penalti yoyote anashinda ni jambo ambalo liko wazi, wachezaji wangu walijituma sana,”alisisitiza Micho.

No comments:

Post a Comment