Saturday, 14 December 2013
HENRY ASEMA ARSENAL INAWEZA KUCHEZA NA YEYOTE
KWANINI waogope? Arsenal inaweza kucheza na timu yoyote. Ndivyo anavyoamini mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Thierry Henry, baada ya timu hiyo kujichongea kwa kushika nafasi ya pili katika kundi lake la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Jumatano usiku Arsenal ilijichongea baada ya kufungwa 2-0 na Napoli nchini Italia na sasa inaweza kujikuta inapangwa na mmoja wa vigogo wa soka barani Ulaya kama vile Bayern Munich, Barcelona, Real Madrid na nyinginezo.
Henry ambaye kwa sasa anafanya mazoezi na kikosi cha Arsenal kwa ajili ya kujiweka fiti wakati huu wa mapumziko ya Ligi Kuu Marekani anakokipiga katika klabu ya New York Redbull, amedai kwamba kwa sasa kikosi cha kocha, Arsene Wenger, kinaweza kucheza na timu yoyote barani Ulaya.
"Nakumbuka mwaka ambao tulifika fainali. Kila mmoja alicheka wakati tulipopangwa kucheza na Real Madrid. Nakumbuka maofisa wao waliondoka wakisema kwamba wana furaha wamepangwa kucheza na Arsenal. Hata hivyo tuliwafunga," alisema Henry.(P.T)
"Mechi iliyofuata tulikwenda kwa Juventus na kila mtu alisema ilikuwa mechi rahisi kwao, lakini pia tulipita. Kuna wakati inabidi uzifunge timu kubwa. Huwezi kutaka kucheza nazo mapema katika hatua za makundi lakini ndivyo ilivyo."
Henry pia alikiri kwamba angependa kucheza timu moja na kiungo mpya wa Arsenal, Mesut Ozil, ambaye amemlinganisha na staa wa zamani wa timu hiyo, Robert Pires.
"Ningependa kucheza naye. Ananikumbusha Robert Pires. Ni aina ya mchezaji ambaye kama ukimpa mpira anakurudishia. Kama ukienda kushoto atakupatia, ukienda kulia bado atakuwepo. Anaweza kumtafuta mchezaji mwenye kasi uwanjani au aliye katika nafasi nzuri na kumpatia mpira anaoutaka," aliongeza.
"Muda wote anaonekana ana muda mwingi wa kutafakari. Anacheza kama vile yupo katika bustani nyumbani kwake na hakuna aliye karibu yake. Inashangaza lakini huyo ndiye mchezaji ambaye unamtaka. Unahitaji utulivu ukiwa na mpira na hicho ndicho alicholeta katika klabu ya Arsenal."
Arsenal leo Jumamosi mchana ina mtihani mkubwa wakati itakaporudi katika pambano la Ligi Kuu England dhidi ya Manchester City ugenini katika Uwanja wa Etihad.
Chanzo:Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment