NA TANZANIA DAIMA
MICHUANO ya Kombe la Chalenji kwa nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), imefikia tamati jana mjini Nairobi, Kenya.
Tanzania, kwa sura ya Jamhuri ya Muungano, ilikuwa na timu mbili kwenye michuano hiyo ambazo ni Kilimanjaro Stars ya bara na Zanzibar Heroes kwa upande wa visiwani.
Wakati Zanzibar Heroes ikiaga michuano hiyo mapema, Kilimanjaro Stars chini ya kocha wake Jan Poulsen ilifika hadi hatua ya nusu fainali kabla ya kufungwa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Kenya yaani Harambee Stars.
Baada ya kufungwa katika hatua hiyo, Kilimanjaro Stars ikaangukia kwenye mechi ya kuwania nafasi ya mshindi wa tatu dhidi ya waalikwa Zambia huku wenyeji Kenya wakicheza mechi ya fainali dhidi ya Sudan.
Katika mechi ya mshindi wa tatu, Kilimanjaro Stars walifungwa na Zambia kwa penalti, hivyo kumaliza michuano hiyo yenye historia ndefu zaidi Afrika tangu mwaka 1926, bila zawadi zilizotolewa kuanzia kwa mshindi wa kwanza hadi wa tatu.
Sisi Tanzania Daima tukiwa sehemu ya wadau wa michezo na maendeleo kwa ujumla, tunawapongeza wachezaji, benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kim na viongozi wa timu hiyo kwa ujumla kwa juhudi walizofanya kuhakikisha timu inapata ushindi.
Tunasema haya kwa kuzingatia kuwa soka ni mchezo wa makosa hivyo kosa moja linaweza kuigharimu timu katika mashindano, lakini vijana walipambana kuanzia hatua ya makundi, robo fainali hadi kutinga nusu fainali ya michuano hiyo.
Tunaamini kitendo cha kufungwa na Kenya pia na Zambia, kitakuwa kimewauma wachezaji, benchi la ufundi na viongozi kwani walipigana vilivyo kama si kubeba ubingwa, basi iwe nafasi ya pili au ya tatu ili kurejea nyumbani na zawadi.
Lakini, hali ya mambo imekuwa tofauti kwani malengo ya kubeba ubingwa wa michuano hiyo iliyohitimishwa jana na kuweka rekodi ya kung’ara kwa mara ya tatu tangu mwaka 1973, yameshindwa kutimia kutokana na sababu kadha wa kadha.
Tunaandika maoni haya kuwatia moyo wachezaji wa timu hiyo kwamba kamwe wasivunjwe moyo na matokeo ya Nairobi, badala yake wachezaji na benchi la ufundi wafanyie kazi dosari zilizofanya washindwe kufikia lengo la ubingwa.
Kama hilo litafanyika, litakuwa jambo la maana kwa mustakabali wa timu hiyo na soka ya Tanzania kwa ujumla hasa ikizingatia kuwa, baada ya michuano hiyo nyota hao hao ndio wataungana na wenzao wa Zanzibar Heroes kuunda kikosi cha Taifa Stars.
Tunasema kama dosari zilizoigharimu timu katika michuano ya Chalenji zitafanyiwa kazi ipasavyo, utakuwa mwanzo mzuri wa kujenga kikosi bora zaidi cha Stars kuelekea kampeni za kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika za 2015.
Ni jukumu la uongozi mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Idara yake ya Ufundi kuja na mikakati sahihi ya nini kifanyike ili ushiriki wa Stars katika kampeni za fainali hizo, uwe wa mafanikio badala ya kubahatisha kila mwaka.
Tunasema haya tukizingatia kuwa kama uongozi wa Malinzi utaendelea kushiriki tu kampeni bila mipango ya kuhakikisha nchi inapata tiketi ya fainali, mambo yataendelea kuwa hivyo huku tukibaki kulaumiana tu, chonde wahusika waamke wachukue hatua.
Tunamaliza kwa kusema wazi hatua ya shirikisho hilo chini ya Malinzi kuwakutanisha makocha wa soka kwa lengo la kubuni mikakati mipya ya nini kifanyike ili kulitoa soka letu hapa lilipo, ni jambo jema na mwanzo mzuri unaoweza kuleta matokeo chanya.
No comments:
Post a Comment