Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Tuesday, 15 October 2013

uchaguzi TFF,RICHARD RUKAMBURA AFUNGIWA MIAKA 20,SHAFFIH NA WILFRED WAPIGWA FAINI



Wilfred Kidau (nyuma ) na Shaffih Dauda

Kamati ya Rufani ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewaadhibu walalamikiwa watano kati ya saba baada ya kufanya mapitio (revision) kwa uamuzi wa Kamati ya Maadili kutokana na maombi ya Sekretarieti, huku Richard Julius Rukambura akifungiwa miaka 20 kujihusisha na mpira wa miguu.

Sekretarieti ya TFF iliwasilisha maombi ya mapitio kwa Kamati ya Rufani ya Maadili ili kupata mwongozo kwa vile kulikuwapo mkanganyiko kwenye uamuzi wa Kamati ya Maadili, hivyo kuiwia vigumu kwake kuutekeleza.

Uamuzi huo wa mapitio umesomwa leo jioni (Oktoba 15 mwaka huu) mbele ya waandishi wa habari na wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Victoria Makani.(P.T)


Rukambura amefungiwa miaka 20 baada ya kupeleka masuala ya mpira wa miguu katika mahakama za kawaida kinyume na Ibara ya 75 ya Katiba ya TFF na kifungu cha 73(3)(b) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013. Adhabu yake itamalizika Oktoba 15, 2033.

Kabla ya kutoa adhabu hiyo, Kamati imejiridhisha kuwa Rukambura ni mwanafamilia wa TFF kwa vile aliwahi kuwa Mwenyekiti wa klabu ya Pamba ya Mwanza, na fomu zake za kuomba uongozi TFF ziliidhinishwa na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga. Vilevile ni 'Leadership Aspirant' kwa mujibu wa kifungu cha 2(v) cha Kanuni za Utii za TFF toleo la 2013.

Pia imesema kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo kusajili Katiba ya TFF inayokataza masuala ya mpira wa miguu kwenda katika mahakama za kawaida, na kutaja vyombo vya haki vitakavyoshughulikia masuala hayo (judicial organs), Kamati ya Maadili ilikosea kutomtia hatiani mlalamikiwa kwa kuegemea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naye Shaffih Dauda, Kamati imebaini kuwa mwanafamilia wa TFF kwani ni Mwenyekiti wa Bombom FC, fomu yake ya kuomba uongozi ilipitishwa na klabu ya Simba na pia ameshakuwa kiongozi katika ngazi mbalimbali ndani ya Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA), hivyo yeye ni 'Leadership Aspirant' kwa mujibu wa kifungu cha 2(v) cha Kanuni za Utii za TFF toleo la 2013.

Hivyo Dauda amepatikana na kosa la kimaadili kwa kutotekeleza maagizo rasmi ya TFF ya kutosambaza barua iliyotoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga.

Kamati ya Rufani ya Maadili imempa onyo kali na faini ya sh. milioni moja anayotakiwa kuilipa ndani ya siku tatu ambapo akishindwa kufanya hivyo atafungiwa mwaka mmoja. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 6(1)(a),(c) na (h) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.

Akilipa faini ataweza kuendelea na mchakato wa kugombea nafasi ya uongozi aliyoomba.

Nazarius Kilungeja amepatikana na kosa la kimaadili kwa mujibu wa kifungu cha 73(8)(a) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013, kwani akijua kuwa ana adhabu ya kinidhamu ya kufungia miaka mitano na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) iliyoanza 2009 alichukua fomu kuomba uongozi TFF.

Hivyo, amefungiwa miaka mitatu, adhabu ambayo itakwenda sambamba na ile ya RUREFA ambapo kifungo chake sasa kitamalizika Oktoba 15, 2016.

Sekretarieti ya TFF imepewa onyo kali kwa kupokea fomu yake ya kugombea na malipo wakati akiwa amefungiwa. Onyo hilo pia limetolewa kwa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) Mkoa wa Rukwa kwa kuidhinisha fomu yake ya kugombea.

Naye Wilfred Kidao Mzigama ambaye ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF amepatikana na kosa la kimaadili kwa kuwa na nyaraka la Kamati ya Utendaji bila kibali na kukiuka taratibu za kuwasilisha malalamiko kwa mujibu wa Ibara ya 12(2) na Ibara ya 50(1) na (5) ya Katiba ya TFF.

Amepigwa faini ya sh. milioni moja anayotakiwa kuilipa ndani ya siku tatu ambapo akishindwa atafungiwa mwaka mmoja. Akitekeleza adhabu hiyo ataweza kuendelea na mchakato wa kugombea uongozi kwa nafasi aliyoomba.

Vilevile Kamati hiyo imetoa onyo kali kwa Sekretarieti ya TFF na wajumbe wa Kamati ya Utendaji kwa kushindwa kudhibiti nyaraka muhimu za vyombo vyao.

Pia Kamati ya Rufani ya Maadili imempata na kosa la kimaadili Kamwanga Tambwe kwa mujibu wa kifungu cha 73(8) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013, kwa kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi wakati ana adhabu ya kinidhamu inayomalizika 2014.

Hivyo, amepewa adhabu ya kufungiwa miaka mitatu ambayo itakwenda sambamba na ile ya kinidhamu na kumalizika Oktoba 15, 2016. Pia Sekretarieti ya TFF, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Ruvuma (FARU) na Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) Mkoa wa Ruvuma wamepewa onyo kali kwa kupokea na kuidhinisha fomu zake za kugombea uongozi wakati akitumikia adhabu ya kufungiwa.

Kamati ya Rufani ya Maadili imewakuta kutokuwa na hatia ya makosa ya maadili kama ilivyobaini Kamati ya Maadili walalamikiwa Riziki Juma Majala na Omar Isack Abdulkadir, hivyo wana haki ya kugombea uongozi kwa kufuata Katiba na Kanuni za TFF.

Kwa mujibu wa kifungu cha 74(4) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013, uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Maadili hauna fursa ya rufani wala marekebisho kutoka chombo kingine chochote isipokuwa FIFA na Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).

chanzo: shafiidauda.com

No comments:

Post a Comment