Wednesday, 1 January 2014
WANACHAMA WAMTAKA RAGE KUACHA UBABE
MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, ametakiwa kuacha ubabe na kujipima katika uongozi wake, ikiwa ni pamoja na kuitisha mkutano wa dharura badala ya kukejeli na kuonyesha umwamba.
Hayo yamesemwa jana na Mwenyekiti wa tawi la New Mapambano, lililopo Temeke, jijini Dar es Salaam, Albino Lwira kwa kushirikiana na wanachama mbalimbali wa klabu hiyo, katika mkutano na wana habari, akiwa na kadi namba (87) iliyotolewa na klabu hiyo.
Akizungumza mbele ya waandishi wa Habari, Lwira alisema kiujumla Rage amevunja katiba ya Simba, kwa kushindwa kuziba nafasi ya Makamu Mwenyekiti aliyejiuzulu miezi minne iliyopita, jambo ambalo linapingwa na katiba yao.
Alisema Rage anasisitiza kuwa anafuata Katiba ya Simba, inashangaza kuwa yeye mwenyewe ameshindwa kuifuata katiba sanjari na kuongoza kiubabe, huku akishindwa kuwasikiliza viongozi wa juu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF).
"Hatuwezi kukaa kusubiri Rage aendelee kuikanyaga Katiba ya klabu yetu kwa faida yake binafsi, hivyo sisi kama wanachama wa Simba tumeumizwa na hatua ya TFF kwa kupitia Kamati ya Maadili na Hadhi za Wachezaji kumsafisha Rage.
"Hii inazalisha chuki na uhasama, maana wamefanya hivyo kwasababu za kumuogopa badala ya kuangalia mahitaji ya wengi sambamba na kusimamia Katiba," alisema Lwira.
Naye Mwanachama maarufu wa Simba, Chuma Seleman maarufu kama Bi Hindu, alisema inashangaza kwanini Rage anaogopwa hata kama anasigina Katiba iliyomuweka madarakani.
"Huu ni ufedhuli wa aina yake na sisi Simba hatuwezi kukubali, kumuona Rage anafanya anavyotaka kwasababu tangu mwanzo amekuwa akiongoza kwa ubabe ," alisema Bi Hindu.
Madai ya wanachama hao, yanaongeza joto kwa wale wanaomtaka Rage aitishe mkutano wa dharura kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya klabu yake, ikiwa ni njia muafaka ya kuiletea mafanikio katika michuano ijayo itakayoanza baadaye mwezi huu. Chanzo: mtanzania
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment