Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
MSHAMBULIAJI tegemeo wa Yanga SC, Mrisho Khalfan Ngassa anasumbuliwa na homa ya matumbo, typhoid ambayo inaweza kumfanya akose michuano ya Kombe la Mapinduzi, inayotarajiwa kuanza wiki hii visiwani Zanzibar.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Ngassa alisema kwamba baada ya kuona hali yake si nzuri kiafya juzi alikwenda kupimwa na akakutwa na maradhi hayo.
“Nimepatiwa tiba na sasa hivi nipo katika dozi, nadhani nitahitaji angalau wiki mbili za kupumzika ili niwe sawa kabisa. Kwa ujumla nimekuwa nikijisikia vibaya kwa muda mrefu tu, ila nikawa nakula dawa za kutuliza maumivu,”alisema Ngassa.
Anaumwa typhoid; Mrisho Ngassa anahitaji kiasi cha wiki mbili kupumzika kutokana na kusumbuliwa na homa ya matumbo
Yanga SC wamepangwa Kundi C katika Kombe la Mapinduzi, michuano itakayoshirikisha timu 12, pamoja na mabingwa watetezi, Azam FC, Tusker ya Kenya na Unguja Combine.
Kundi kuna Mbeya City, Pemba Combine, Chuoni na URA kutoka Uganda wakati Kundi B lina timu za Simba SC, KMKM, AFC Leopards ya Kenya na KCC ya Uganda.
Pazia la ngarambe hizo litafunguliwa Januari 1, 2014, kwa mechi mbili za kundi B katika uwanja wa Amaan, ambapo wakati wa saa 10:00 mabaharia wa KMKM watapambana na Manispaa ya jiji la Kampala (KCC).
Aidha saa 2:00 usiku, wekundu wa Msimbazi Simba SC, watakuwa kibaruani dhidi ya AFC Leopards.
Januari 2, 2014, kutakuwa na mechi nne, katika kila uwanja, kati ya Amaan Unguja na Gombani Pemba, kutakuwa na michezo miwili.
Zile za Amaan, ni kati ya Azam FC na Unguja Combine (saa 10:00 jioni) na Yanga dhidi ya Tusker itakayorindima kuanzia saa 2:00 usiku, na huko Gombani shughuli itakuwa kati ya URA na Chuoni (kundi C) watakaovaana saa 8:00 mchana, huku Mbeya City ikitoana jasho na Pemba Combine, saa 10:00 jioni katika mchezo wa kundi A.
Fainali ya ngarambe hizo itapigwa uwanja Amaan Januari 12 wakati wa saa 2:00 usiku, ambayo ndiyo kilele cha maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment