Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Thursday 26 December 2013

Logarusic: Mkinipa Yanga nafukuza mabeki wote



Kocha Mkuu wa Simba,Zdravko Logarusic.PICHA|MAKTABA
KOCHA Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic, amempa pole mwenzake wa Yanga, Ernest Brandts, kwa kupewa notisi na uongozi wa timu hiyo, lakini akasema angekuwa anaifundisha Yanga angewatimua mabeki wanne wa kikosi hicho wakiwamo nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani.
Logarusic ameliambia Mwanaspoti kuwa safu ya ulinzi ya timu hiyo ndiyo tatizo kubwa na ndio maana akaichapa Yanga mabao 3-1 katika mechi ya Nani Mtani Jembe wiki iliyopita. Amesisitiza kuwa tatizo si kocha Brandts.


Mabeki waliokuwa kwenye ukuta wa Yanga katika mechi hiyo, kulia alicheza Mbuyu Twite, kushoto alikuwa David Luhende na katikati walisimama Cannavaro na Yondani.


Logarusic alisema mabeki hao pamoja na kiungo mkabaji wa siku hiyo, Athuman Idd ‘Chuji’, walishindwa kutekeleza majukumu yao ambapo waliruhusu washambuliaji wa Simba kuuona uso wa goli, tofauti na kazi waliyofanya mabeki wake, Mkenya Donald Musoti na Joseph Owino raia wa Uganda.


Mcroatia huyo aliongeza kuwa yeye hana tabia ya kuwavumilia wachezaji wanaofanya masihara ya wazi uwanjani ambayo yanaweza kuhatarisha ulaji wake na ndio maana anapogundua mchezaji anakosa umakini, hakawii kumrudisha benchi au jukwaani.


“Nimesikia wamemfukuza (Brandts) nampa pole kwa hilo, lakini haya ndio maisha yetu makocha, hakuna cha ajabu. Sasa imetokea kwake na siku nyingine unaweza kusikia kwangu,” alisema.


“Lakini najua ni kutokana na matokeo dhidi ya Simba. Ningekuwa naifundisha Yanga ningewafukuza mabeki wote waliocheza katika mchezo ule. Ukiangalia kwa makini walivyokuwa wakicheza huwezi kuamini kama kweli wale ni mabeki, walikuwa wakifanya makosa mengi ya kushangaza.


“Wewe ni beki unaruhusu vipi mshambuliaji kupata nafasi ya kuuona uso wa goli? Sipendi kuona beki anafanya makosa kama yale unaona jinsi Musoti na Owino walichokuwa wakikifanya? Ndivyo mabeki wanavyotakiwa kufanya.


“Ikitokea beki wangu anafanya uzembe kama ule wa wale wa Yanga naweza kuwaondoa haraka na kama nikikasirika zaidi naweza hata kuwatimua kabisa.”


Katika hatua nyingine, juzi Jumanne wachezaji wa Yanga walikabidhiwa kitita cha Sh50 milioni zikiwa ni salio lililokuwa limebakia kwenye zawadi ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.


Habari ambazo Mwanaspoti imepata, zinasema kuwa wachezaji hao walikabidhiwa fedha hizo ikiwa ni ahadi ya Mwenyekiti, Yusuf Manji, ambaye aliwaahidi Sh100 milioni endapo watashinda mechi tano za mwishoni mwa msimu huo na kutwaa ubingwa, jambo ambalo walilitimiza.


Mwishoni mwa msimu uliopita, wachezaji hao walipewa Sh50 milioni wagawane jambo ambalo halikuwafurahisha sana kwani walihisi viongozi wao ni wababaishaji.

No comments:

Post a Comment