Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Saturday, 28 September 2013

MAKALA Siri Yanga matokeo ya Ligi Kuu Bara





By MWANDISHI WETU
Matokeo hayo yanaifanya Yanga iwe imepigwa mabao sita kwenye mechi tano licha ya kuwa na mabeki mahiri wanne ambao wanacheza kwenye timu za Taifa ambao ni Cannavaro, Twite, Yondani, Luhende na Barthez

YAKUMBUKE kwanza majina haya; Cannavaro, Twite, Yondani, Luhende na Barthez. Halafu endelea kusoma habari hii.

Kuna timu nne pekee za Tanzania zinazofanya matumizi makubwa zaidi msimu huu ikiwamo kulipa mishahara mikubwa na kuishi kifahari. Ni Yanga, Azam, Simba na Coastal Union. Lakini timu hizo zimeiachia Yanga manyoya.


Yanga imeachwa vibaya kwenye mambo mawili. Kwanza; ndiyo timu pekee iliyoshinda mchezo mmoja tu tena dhidi ya timu dhaifu ya Ashanti United ambayo kila mtu anajipigia nyumbani na ugenini.


Lakini, pili; Yanga ambayo ina asilimia 90 ya kikosi kilichotwaa ubingwa msimu uliopita ndiyo timu pekee katika vigogo hao iliyoruhusu bao katika kila mechi kwani katika mechi zake tano imepigwa mabao sita.


Ilianza kwa kuichapa Ashanti mabao 5-1, ikatoka sare tatu za bao 1-1 dhidi ya Coastal Union, Mbeya City na Prisons kabla ya kufungwa na Azam mabao 3-2 mwishoni mwa wiki.


Yanga imecheza mechi mbili nje ya Dar es Salaam na kuruhusu mabao mawili.


Matokeo hayo yanaifanya Yanga iwe imepigwa mabao sita kwenye mechi tano licha ya kuwa na mabeki mahiri wanne ambao wanacheza kwenye timu za Taifa ambao tulikutaka uyakumbuke majina yao hapo juu. Nadir Haroub Cannavaro, Mbuyu Twite, Kelvin Yondani, David Luhende na kipa wao namba moja, Ally Mustapha ‘Barthez’.


Kocha wa Yanga, Ernest Brandts amekiri kwamba: “Ni uzembe ambao umekuwa ukitokea kila mara na wenzetu wanatumia nafasi hizo, tumeliona hilo na tumeanza kulifanyia kazi kwa kufanya mabadiliko fulani kwenye safu yetu ya ulinzi. Lakini vilevile unapaswa kujua kwamba ligi ni ngumu na bado inaendelea.”


Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi alisema:


“ Yanga ni waoga wanacheza mipira mirefu, kama kule Mbeya hawakucheza kabisa, sijui ni kwasababu ya uwanja kama walivyosema au la. Lakini hata kama uwanja mbovu wajitahidi kucheza mpira.”


Kiongozi mmoja wa Yanga alikiri jana Jumatatu kuwa wanachunguza kuona kama kuna jambo lolote katika timu hiyo.


“Tumecheza mchezo mzuri dhidi ya Azam, lakini tukafungwa, tunalifanyia kazi hilo kuona kama kuna kitu chochote,” alisema.Azam imecheza tatu mechi nje ya Dar es Salaam na kuruhusu mabao mawili. Imetoka sare za bao 1-1 kwenye mechi dhidi ya Mtibwa, Kagera Sugar na ikaifunga Rhino mabao 2-0. Katika mechi za Dar es Salaam imetoka sare ya bao 1-1 na Ashanti United na ikaifunga Yanga mabao 3-2.
Simba imecheza mechi tano na kuruhusu mabao mawili mkoani katika sare ya mabao 2-2 dhidi ya Rhino, ikapata sare kama hiyo dhidi ya Mbeya City, ikaichapa JKT Oljoro bao 1-0, ikailaza Mtibwa mabao 2-0 na kuishukia Mgambo JKT mabao 6-0. Kipigo cha mabao 6-0 ndiyo kikubwa zaidi kwenye ligi inayoendelea sasa.
MBINU ZA SIMBA
Katika hatua nyingine, Mwambusi amesema kuwa mashambulizi ya pembeni kupitia kwa mabeki wa kulia na kushoto wanaopanda kupiga krosi kwa mastraika na viungo ndio roho ya Simba.
Kocha huyo aliligundua hilo mapema, akaziba njia na ndiyo sababu ya kurudisha mabao yote mawili waliyokuwa wamefungwa na Simba na kulazimisha sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.
Simba huwachezesha, Rashid Issa ‘Baba Ubaya’ beki ya kushoto na kulia, Nassor Said ‘Cholo’ ambaye katika mchezo huo hakuwepo kutokana na majeruhi na nafasi yake ilichezwa na William Lucian ‘Gallas’.
Mwambusi kocha wa zamani wa Moro United na Prisons ya Mbeya alitumia fomesheni ya 4-4-2 sawa na Simba na kutokana na mbinu hizo Simba ilipandisha mashambulizi zaidi kupitia kulia kwa Gallas aliyekuwa anamtesa beki wa kushoto wa Mbeya City, Hassan Mwasapili.
Jambo ambalo Mwambusi alilishtukia na kuongeza ulinzi, akaziba njia kwa kuboresha winga yake ya kushoto akamtoa, Yusuph Wilson na kumuingiza, Richard Peter mfungaji wa bao la pili ambaye pia, baadaye alihamia kulia na Deus Kaseke aliyekuwa anacheza kati akabaki kushoto.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwambusi alisema: “Nafahamu Simba nguvu yao ni kwa mabeki wa pembeni katika kutafuta mabao, mabeki hao hupanda na kucheza kama mawinga halafu wanapiga krosi kwa mastraika na viungo wanaokuwa hapo.”
“Na ndivyo walivyotufanyia sisi kipindi cha kwanza, walikuwa wasumbufu sana kwenye ‘fulubeki’ zao hasa kulia, walisumbua sana upande wetu wa kushoto katika kupandisha mashambulizi, kulia haikuwa shida sana,” alisema Mwambusi.
“Na tulipoenda mapumziko tukaulizana maswali na kuelekezana, tukajipanga na tatizo kwanza lilikuwa vipimo vya uwanja kama unavyojua ni mara ya kwanza wanautumia Uwanja wa Taifa.”
Ratiba ijayo
Yanga itakuwa na mtihani mwingine itakapocheza na Ruvu Shooting Jumamosi wakati Simba itacheza na JKT Ruvu Jumapili, mechi ambazo zitachezwa Dar es Salaam.www.tabasamuleo.blogspot.com

No comments:

Post a Comment