Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Saturday, 8 March 2014

RAHISI NGAMIA KUPENYA TUNDU LA SINDANO KULIKO AL AHLY KUITOA YANGA LEO

CHANZO; NA BIN ZUBEIRY
YANGA SC usiku wa leo inashuka kwenye Uwanja wa Border Guard, Alexandria nchini Misri kumenyana na wenyeji, Al Ahly katika mchezo wa marudiano, Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga itamenyana na mabingwa hao wa Afrika, ikiwa kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele, kufuatia ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza nyumbani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Suala si ushindi tu, kiwango ambacho walichoonyesha Yanga SC Jumamosi ya wiki iliyopita na aina ya uchezaji wa kushambulia kwa kasi ndiyo vitu vinavyotia matumaini zaidi, hasa baada ya kocha wa timu hiyo, Mholanzi, Hans van der Pluijm kusema watarudia kucheza namna hiyo leo.


Hata kama Yanga SC watacheza mchezo wa kujihami zaidi, bado watakuwa tishio kwa Ahly kwa kuhofia wanaweza kufungwa kwa mashambulizi ya kushitukiza.Al Ahly iliwaona washambuliaji wa Yanga SC wote walivyo na kasi na uwezo wa kumiliki mpira katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam na itaendelea kuwahofia Waganda Emmanuel Okwi, Hamisi Kiiza, wazalendo Mrisho Ngassa, Simon Msuva na Mrundi Didier Kavumbangu.
Ndiyo, Ahly nao walitengeneza nafasi na Amr Gamal alipiga mashuti mawili yaliyookolewa na kipa Deo Munishi ‘Dida’, lakini bado siku hiyo Yanga SC ndiyo walikuwa hatari zaidi uwanjani.
Wazi kama Yanga SC watarudia kucheza mchezo mzuri kesho, wanaweza kufanya kile ambacho wengi hawatarajii kuwatoa Ahly, ambao hawajawahi kutolewa na timu yoyote ya Tanzania kwenye michuano ya Afrika.
Kihistoria, Machi 1, 2014 ilikuwa mara ya kwanza kabisa Yanga SC inapata ushindi dhidi ya timu ya Misri na Kaskazini mwa Afrika kwa ujumla, kwani mara zote imekuwa ikifungwa na kutoa sare.
‘Bismillah’ Yanga inakutana kwa mara ya kwanza na Al Ahly na timu za Kaskazini kwa ujumla ilikuwa ni mwaka 1982 katika Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa na katika mchezo wa kwanza mjini Cairo, Waarabu hao walishinda 5-0 na marudiano Dar es Salaam timu hizo zikatoka sare ya 1-1.
Zikakutana tena mwaka 1988 katika Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa mchezo wa kwanza ukimalizika kwa sare ya bila kufungana Dar es Salaam wakati marudiano mjini Cairo, Yanga wakabebeshwa 4-0.
Mara ya mwisho Yanga kukutana na Ahly kabla ya Machi 1, 2014 ilikuwa mwaka 2009 katika Raundi ya Kwanza pia Ligi ya Mabingwa pia na mchezo wa kwanza Cairo, wakafungwa 3-0 wakati marudiano Dar es Salaam wakafungwa pia 1-0.
Historia imeandikwa, Machi 1, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga SC wamepata ushindi wa kwanza kabisa dhidi ya Ahly na timu za Kaskazini kwa ujumla na leo Uwanja wa Border Guard Yanga watajaribu kuitoa mashindanoni kwa mara ya kwanza kabisa timu ya Kaskazini mwa Afrika tangu ianze kukutana nazo 1982.
Ukweli ni kwamba, si jambo jepesi kuitoa timu ya Misri au Kaskazini mwa Afrika kwa mtaji wa ushindi wa 1-0 nyumbani- Simba SC waliifunga Haras El Hodoud 2-1 Dar es Salaam wakaenda kupigwa 5-0 Alexandrie.
Lakini mchezo wa leo ni mgumu mno kwa Ahly na utakuwa mwepesi iwapo watafanikiwa kupata bao ndani ya dakika 10 za mwanzo, kitu ambacho Yanga SC wanatakiwa kuchunga sana.
Yanga SC wanatakiwa kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu leo, kujituma na kuwa makini muda wote. Wachezaji wachunge kupewa kadi hata za njano, kwani kutawafanya wacheze kwa woga kwa watakaopewa kadi kwa kuhofia kuonyeshwa ya pili na kutolewa uwanjani, hivyo kuwapa nafasi Ahly kuulazimisha mchezo watakavyo.
Kulingana na kiwango cha Yanga SC Dar es Salaam na kama watarudia kucheza vizuri na leo pia ugenini, itakuwa rahisi kwa ngamia kupenya kwenye tundu la sindano kuliko Al Ahly kuwatoa mabingwa hao wa Tanzania. Kila la heri Yanga SC, Mungu ibariki Yanga SC, ibariki Tanzania. Amin.

No comments:

Post a Comment