Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Monday 3 March 2014

AZAM KUMSAJILI MFUNGAJI BORA KOMBE LA MAPINDUZI, KOCHA OMOG ATOA BARAKA ZOTE

Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
MFUNGAJI bora wa michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu, Mganda Owen Kasule amefuzu majaribio katika klabu ya Azam FC na sasa atasajiliwa kwa ajili ya msimu ujao.
Kocha Mcameroon Joseph Marius Omog ameridhishwa na uwezo wa kiungo huyo mshambuliaji wa URA ya Uganda baada ya majaribio ya wiki mbili na ameuambia uongozi umsajili.

Kifaa kipya Chamazi; Kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Owen Kasule atasajiliwa Azam FC baada ya kufuzu majaribio
Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Idrissa ‘Father’ ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, kocha Omog baada ya kuridhishwa na uwezo wa mchezaji huyo wa kimataifa wa Uganda, amependekeza apewe Mkataba na suala hilo sasa lipo kwenye uongozi.
Kasule alirejea nyumbani mwaka jana kujiunga na timu ya Mamlaka ya Mapato Uganda (URA) baada ya kuichezea kwa msimu mmoja (2012) Hoang Anh Gia Lai ya Vietnam.
Owen Kasule aliyezaliwa Machi 3 mwaka 1989, kisoka aliibukia klabu ya Kampala City Council (KCC FC) na amekuwa akicheza Ligi Kuu ya Uganda tangu msimu wa 2006-2007 kabla ya kuhamia Bunamwaya aliyoichezea hadi anakwenda Vietnam.
Katika maendeleo mengine, Nassor Father amesema kwamba kiungo Joseph Lubasha Kimwaga aliyekuwa majaeruhi anaendelea vizuri baada ya tiba na yuko katika wiki ya mwisho ya mapumziko, kabla ya kuanza mazoezi mepesi.
Father amesema beki Waziri Salum na kiungo Farid Mussa Malik wamepona kabisa na wamekwishaanza mazoezi.
Na kuhusu mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyerejea uwanjani hivi karibuni baada ya kuwa nje kwa muda mrefu sababu ya majeruhi pia, Father amesema naye anaendelea vizuri akipambana kurudi katika kiwago chake.
Azam FC baada ya kutolewa katika Hatua ya Awali ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF), sasa imeelekeza nguvu zake katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambako inaongoza ligi hiyo hadi sasa kwa pointi zake 40, ikifuatiwa na Yanga SC yenye pointi 38, lakini ina mechi moja mkononi.

No comments:

Post a Comment