Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
YANGA SC imetoa onyo kwa wapinzani wao katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwezi ujao, Al Ahly ya Misri baada ya kuifumua mabao 7-0 Ruvu Shooting ya Pwani katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii.
Ushindi huo unaifanya Yanga SC irejee kileleni mwa Ligi Kuu baada ya kutimiza pointi 38, mbili zaidi ya Azam inayoangukia nafasi ya pili sasa, ambayo kesho itamenyana na Prisons ya Mbeya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Wawili wabaya; Emmanuel Okwi kulia na Mrisho Ngassa wakishangilia baada ya bao la nne leo na chini Kavumbangu anapongezwa baada ya kufunga moja ya mabao yake
Hadi mapumziko, tayari Yanga SC walikuwa mbele kwa mabao 4-0 yaliyotiwa kimiani na Didier Kavumbangu, Simon Msuva, Emmanuel Okwi na Mrisho Ngassa.
Yanga SC leo ilibadilika mno kiuchezaji na kuonyesha soka ya kiwango cha juu, tofauti na soka yao iliyozoeleka ya bila mipango inayosababisha kupoteza nafasi nyingi.
Ngassa alicheza nafasi ya kiungo mchezeshaji mbele ya mkabaji Frank Domayo na kuiongoza vyema timu, hata kuwa chachu ya ushindi huo mnono.
Kavumbangu alifunga dakika ya kwanza kwa shuti kali baada ya kupokea pasi ya Okwi, wakati Msuva alifunga dakika ya pili kwa shuti pia baada ya pasi ya Ngassa.
Okwi aliifungia Yanga dakika ya 28 baada ya pasi ya Hamisi Kiiza na kumlamba chenga kipa Abdallah Ramadhani na dakika mbili baadaye, Ngassa akafunga la nne baada ya kumtoka beki Mangasini Mbonosi.
Kipindi cha pili, Yanga SC ilirudi na moto wake na kupata mabao matatu zaidi. Kavumbangu alifunga bao la tano dakika ya 53 akimalizia krosi ya Msuva.
Mganda Hamisi Kiiza ‘Diego’ alinogesha karamu ya mabao ya Yanga SC leo kwa kufunga bao la sita dakika ya 69 akimalizia pasi ya Msuva.
Nyota wa mchezo wa leo, Msuva alihitimisha karamu ya mabao ya Yanga SC kwa kufunga bao la saba dakika ya 78.
Baada ya mchezo huo, Yanga SC inarejea kambini Bagamoyo, Pwani kuendelea na maandalizi ya mechi yake ya kwanza ya Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Ahly Machi 1, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi mkubwa zaidi kwa Yanga SC katika historia ya Ligi Kuu unabaki kuwa wa mabao 8-0 dhidi ya Kagera Stars (sasa Kagera Sugar) mwaka 1998, siku ambayo Edibily Jonas Lunyamila pekee alifunga mabao matano.
Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Mbuyu Twite/Juma Abdul dk67, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva, Mrisho Ngassa/Hassan Dilunga dk60, Didier Kavumbangu/Said Bahanuzi dk77, Emmanuel Okwi na Hamisi Kiiza.
Ruvu Shooting; Abdallah Ramadhani, Michael Aidan, Stephano Mwasyika, Mangasini Mbonosi, Shaaban Suzan/Gideon Sepodk58, Ali Khan, Hamisi Ismail/Ayoub Kitala dk44, Juma Nade/Said Madegadk34, Elias Maguli, Jerome Lambele na Cosmas Lewis.
Katika michezo mingine ya ligi hiyo leo, Mbeya City wamepunguzwa kasi kwa kulambwa mabao 2-0 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga mabao ya Mohamed Mtindi dakika za 82 na 89.
No comments:
Post a Comment