Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Monday 17 February 2014

Lulu akiri mahakamani kuwa mpenzi wa Kanumba

Dar es Salaam. Mwigizaji maarufu wa filamu nchini, Elizabeth Michael Kimemeta, amekiri mahakamani kuwa na uhusiano wa kimapenzi na aliyekuwa mwigizaji mwenzake, Steven Kanumba na pia kuwa ugomvi na Kanumba siku ya tukio la kifo cha mwigizaji huyo, lakini akakana mashtaka ya kumuua bila kukusudia.
Lulu ambaye yuko nje kwa dhamana anakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akidaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia, kinyume cha Kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu (PC), April 7, 2012, nyumbani kwa marehemu Kanumba, Sinza Vatican.
Jana Lulu alipandishwa kizimbani mahakamani hapo na kujibu mashtaka hayo kwa mara ya kwanza tangu alipofunguliwa kesi hiyo, ambapo alikana kumuua Kanumba bila kukusudia.Kesi hiyo namba 125 ya mwaka 2012 inasikilizwa na Jaji Rose Teemba.

Kukubali kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Kanumba, ni miongoni mwa mambo manane ambayo mshtakiwa huyo aliyakiri mahakamani hapo jana, kama mambo yasiyobishaniwa katika kesi hiyo.

Awali Lulu alisomewa mashtaka hayo na Karani wa Mahakama aliyefahamika kwa jina la Tuvana, kuwa tarehe hiyo alimuua mtu mmoja aitwaye Steven Kanumba bila kukusudia kinyume, na kisha akamuuliza kama ni kweli au si kweli, lakini Lulu akajibu kuwa si kweli.

Baada ya kukana mashtaka hayo, Wakili wa Serikali Monica Mbogo alimsomea maelezo ya kesi hiyo, na kisha Lulu akatakiwa kuainisha mambo anayokubaliana nayo na yale asiyokubaliana nayo.


Katika maelezo hayo, Wakili Mbogo alisema kuwa mshtakiwa na Kanumba walikuwa na uhusiano wa kimapenzi na kwamba mshtakiwa alikuwa na kawaida ya kumtembelea Kanumba nyumbani kwake.


Alieleza kuwa siku ya tukio, saa sita za usiku, Kanumba alimwambia mdogo wake (Seth Bosco) kuwa ajiandae watoke na kwamba wakati wakijiandaa, mshtakiwa alifika nyumbani hapo na kuingia moja kwa moja hadi chumbani kwa Kanumba.


Aliongeza kuwa wakiwa huko chumbani mara Bosco alisikia malumbano baina ya Kanumba na mshtakiwa, huku Kanumba akimlalamikia mshtakiwa kuwa ni kwa nini anasikiliza simu ya bwana wake mbele yake.


Aliendelea kuwa baadaye Bosco alimsikia mshtakiwa akianza kulia na kwamba alisogea karibu na mlango akachungulia na kumuona mshtakiwa akijitahidi kutaka kutoka nje, lakini Kanumba alimvuta na kisha mlango ukafungwa.


Wakili Mbogo aliendelea kuwa baadaye mshtakiwa alitoka nje na akamweleza Bosco kuwa Kanumba ameanguka na kwamba Bosco alipokwenda alimkuta Kanumba ameanguka sakafuni huku akiwa hajimbui.


Alisema kuwa Bosco alimjulisha daktari binafsi wa Kanumba (Paplas Kageiya) kuhusu hali ya Kanumba na kwamba Dk Kageiya alipofika alimkuta Kanumba ameshafariki, lakini hakumweleza Bosco, bali alishauri wampeleke hospitalini.


Wakili Mbogo alieleza kuwa wakati huo mshtakiwa hakuwepo eneo la tukio na kwamba walipofika hospitalini Muhimbili, baada ya kumchunguza Kanumba, ilibainika kuwa alikuwa ameshafariki dunia.


Alibainisha kuwa taarifa ya uchunguzi wa kitabibu kuhusu chanzo cha kifo hicho ilibainisha kuwa marehemu alikufa kutokana tatizo lijulikanalo kwa kitaalamu kama Brain Concussion.

Mambo mengine ambayo Lulu aliyakiri mahakamani hapo yaliyoko katika maelezo ya kesi hiyo ni pamoja na jina na anuani yake, kwenda nyumbani kwa Kanumba usiku wa tukio hilo, kuwa na ugomvi na Kanumba pia Kanumba kumzuia kutoka nje ya chumba alipojaribu kutoka ili akimbie.


Mengine ni kufanikiwa kutoka nje ya chumba cha Marehemu Kanumba, kumweleza mdogo wa Kanumba (Seth Bosco) kuwa Kanumba ameanguka, kukamatwa kwake na polisi eneo la Bamaga, saa 11 Alfajiri ya usiku wa tukio hilo na kwamba kweli anashtakiwa kwa kosa la kumuua Kanumba bila kukusudia.


Kama jana Lulu angekiri mashtaka hayo baada ya kusomewa, basi mahakama ingemtia hatiani na kumhukumu adhabu ambayo ingeona inafaa kwa mujibu wa sheria.


Hata hivyo, baada ya kukana mashtaka hayo, sasa kesi hiyo itaingia katika hatua nyingine ya usikilizwaji kamili (trial), ambapo upande wa mashtaka utalazmika kuwaita mashahidi wake mahakamani ili kuthibitisha kuwa Lulu alimuua Kanumba bila kukusudia.


Pia Lulu atalazimika kujitetea yeye binafsi na pia kuwaita mahakamani mashahidi wa kumtetea na kisha mahakama itaandaa na kutoa hukumu yake.


Wakili wa Serikali, Mbogo aliiarifu mahakama kuwa wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa mashtaka utakuwa na mashahidi wanne ambao ni pamoja na Seth Bosco, Daktari binafsi aliyekuwa akimhudumia Kanumba, Dk Paplas Kageiya, Ester Zephania na Askari D/Sgt Ernatus wa Kituo cha Polisi Oysterbay.


Pia Wakili Mbogo aliwasilisha mahakamani vielelezo viwili vitakayotumika kama sehemu ya ushahidi katika kesi hiyo ambayo ni taarifa ya kitabibu ya uchunguzi wa chanzo cha kifo cha Kanumba na ramani ya eneo la tukio.


Lulu kwa upande wake, mawakili wake Peter Kibatala na Fulgence Massawe waliiarifu Mahakama kuwa wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo kwenye utetezi watakuwa na mashahidi watano na vielelezo viwili. Hata hivyo hawakutaja majina ya mashahidi hao.

No comments:

Post a Comment