Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Tuesday, 11 February 2014

WANA SIMBA SC WAIPENDE TIMU YAO KATIKA WAKATI MGUMU PIA

BAADA ya kuambulia pointi moja katika mechi mbili za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC wanakwenda katika mchezo mwingine mgumu Jumamosi dhidi ya Mbeya City.
Walitoa sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro wakaenda kufungwa 1-0 na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga- sasa wanakwenda Uwanja wa Sokoine kuifuata Mbeya City, nini matarajio?
Naamini hapa hata wana Simba vichwa vinawauma wanapoufikiria mchezo huo, ikizingatiwa Mbeya City ni moja ya timu bora katika Ligi Kuu msimu huu na za ushindani haswa, ambayo bado ipo kwenye mbio za ubingwa.


Ukweli ni kwamba Simba SC wanaingia kwenye mchezo mwingine mgumu na lolote linaweza kutokea, kufungwa, kushinda au kutoa sare kwa sababu Mbeya City ni timu ngumu na siyo tu haijafungwa nyumbani, bali msimu mzima huu wa ligi wamefungwa mechi moja tu Yanga Dar es Salaam tena kwa mbinde, mchezaji wao tegemeo, Steven Mazanda akitolewa kwa kadi nyekundu mapema kipindi cha pili.
Wamesimama imara baada ya kupoteza mechi na Yanga wakashinda dhidi ya Mtibwa Sugar 2-1 na tangu hapo wamekuwa katika maandalizi makini kuelekea mechi na Simba SC.
Ukweli ni kwamba Simba SC wanakabiliwa na mtihani mgumu Jumamosi.
Hali hii inatokea Simba SC ikiwa katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu nyuma ya Azam FC inayoongoza, Yanga SC inayofuatia na Mbeya City katika nafasi ya tatu.
Ukirejea historia ya Simba SC kwa misimu hii miwili pekee imepitia katika vipindi vigumu, ikiwemo kubadilisha makocha na idadi kubwa ya wachezaji.
Inaonekana kabisa Simba SC wanatafuta namna ya kutulia kwanza, kwa maana ya timu na pili kuwa katika hali nzuri kuweza kurudia kwenye makali yake.
Pamoja na mgogoro wa uongozi, zipo jitihada za wazi na zinaonekana kabisa za baadhi ya viongozi ndani ya Simba katika kuhakikisha timu hiyo inaimarika tena.
Pongezi za dhati zimundee Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe ambaye kwa hakika anajitolea kwa hali na mali kwa ajili ya Simba SC bila ya kukata tamaa pamoja na mazingira yote magumu.
Umefika wakati wana Simba SC wafunguke zaidi na waache kuwa na fikra nyepesi juu ya timu yao, watambue ugumu ambao unawakabili ili kurejea kwenye ndoto za ubingwa.
Zile zama za Simba na Yanga kuitawala soka ya Tanzania zitakavyo, wazi sasa zinaelekea ukingoni na itafika wakati timu bora tu ndiyo itakuwa na nafasi ya kuinua taji la ubingwa wa Ligi Kuu.
Azam ipo kileleni, Yanga wa pili, Mbeya City wa tatu na Simba SC wa nne hadi sasa ligi ikiyoyoma, tujipe matumaini timu yoyote kati ya hizo nne inaweza kutwaa taji mwishoni mwa msimu, lakini ukifanya tathmini ya kina unagundua hizi ni mbio za farasi wawili, wa Jangwani na Chamazi.
Ina maana Simba SC inaweza kuwa nje ya michuano ya Afrika kwa mwaka wa pili mfululizo mwakani baada ya mwaka huu pia kupigwa kumbo na Yanga na Azam.
Kwa kawaida, Simba na Yanga zinapokosa nafasi moja kati ya mbili za juu kwenye ligi, mashabiki wake hukasirika sana na kuanzisha vurugu kwenye klabu.
Lakini wana Simba mwaka huu lazima wabadilike na wawe tayari kukubaliana na hali halisi kwamba mambo yamebadilika katika Ligi Kuu na ushindani umeongezeka.
Simba SC imefungwa na Mgambo inayoelekea kushuka Daraja, hii si ajabu kwani timu hiyo huko nyuma ikiwa na vikosi bora vilivyotwaa ubingwa mwisho wa msimu ilifungwa pia na timu zilizoshuka Daraja kama Bandari ya Mtwara, Toto ya Mwanza na Polisi za Morogoro na Dodoma.
Hata Ulaya ipo hiyo, timu inaongoza ligi, inafungwa na timu ambayo inashuka daraja.
Simba SC waiheshimu Ligi Kuu, wakubali mapungufu ya timu yao na wawape fursa viongozi wao waisuke timu hiyo taratibu, kwa sababu wapo katika juhudi endelevu kwa miaka miwili sasa.
Wachezaji wangapi wamesajiliwa Simba SC kwa miaka hii miwili na kutupiwa virago baada ya muda mfupi kufuatia kuonekana hawafai? Yote hiyo ni katika jitihada za kuitafuta Simba nyingine bora.
Tazama Manchester United wanavyopitia katika wakati mgumu hivi sasa England, lakini itafika wakati watatulia na mambo yatakwenda sawa, kwa sababu hii si mara ya kwanza kwao na wamekwishazoea kucheza ligi ya ushindani.
Simba SC nao walitambue hilo, kwamba wapo katika harakati fulani ambazo zinahitaji utulivu wa hali ya juu bila kuvurugana ili kuzifanikisha.
Mashabiki wanaumia kwa matokeo mabaya ni haki yao kwa sababu wanapenda, lakini wao hawatoi hata senti moja, ila kuna wenzao wanaoipenda pia Simba SC ambao wanatoa mamilioni yao kama Hans Poppe kwa ajili ya kuhakikisha siku moja timu hiyo inarejesha hadhi yake.
Watu kama hawa ukijaribu kidogo tu kuwavuruga rahisi sana kukasirika na kuamua kujiweka pembeni na hapo mambo yatavurugika kabisa.
Mashabiki wa Simba SC waonyeshe mapenzi ya dhati kwa kuipenda timu yao katika wakati mgumu pia.
Simba SC hii inaundwa na wachezaji wale wale waliowafunga Yanga SC mabao 3-1 Desemba 21, mwaka jana katika mechi ya Nani Mtani Jembe hadi mashabiki wa timu hiyo wakafurahia sana.
Simba SC hii inaweza kufanya hivyo tena kwa Yanga watakapokutana nayo. Na bado ina nafasi hata ya kutwaa ubingwa, endapo wapinzani watateteleza, ila tu ni iwapo haitovuruwga kwa migogoro. Neno moja tu kwa wapenzi wa Simba leo, waipende timu yao katika wakati mgumu pia. Naitwa Mahmoud Ramadhani Zubeiry, Jumatano njema.

No comments:

Post a Comment