Pages

ELIMU KWANZA.

ELIMU KWANZA.
FEDHA SIO KIPAUMBELE CHETU.

Saturday 15 February 2014

SIMBA SC imegawana pointi na wenyeji Mbeya City baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 Uwanja wa Sokoine Mbeya

Na Mahmoud Zubeiry, Mbeya
Matokeo hayo yanaifanya Mbeya itimize pointi 35 sawa na Yanga SC iliyo nafasi ya pili kwa wastani mzuri wa mabao wakati Simba inatimiza pointi 32 na inabaki nafasi ya nne.
Hadi mapumziko, tayari Mbeya City walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na Deogratius Julius kwa penalti dakika ya 13, akimchambua vizuri kipa Mghana, Yaw Berko.

Wachezaji wa Mbeya City wakishangilia bao la kuongoza kabla ya Simba kusawazisha leo Uwanja wa Sokoine
Penalti hiyo ilitolewa kufuatia beki Joseph Owino kuunawa mpira katika harakati za kuokoa krosi ya Deus Kaseke kutoka wingi ya kushoto.
Mbeya City walitawala mchezo na kipindi cha kwanza na Simba SC ilimtumia Ramadhani Singano ‘Messi’ kushambulia, ambaye hata hivyo aliwekewa ulinzi mkali na mabeki wa timu ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Mshambuliaji Mrundi Amisi Tambwe aliunganishia juu ya lango kwa kichwa mipira miwili ya adhabu iliyopigwa na Amri Kiemba kipindi cha kwanza, kufuatia Messi kuangushwa.


Kipa wa Simba SC, Yaw Berko akiwa amepiga magoti baada ya kufungwa kwa penalti leo Uwanja wa Sokoine


Kocha Mkuu wa Simba SC, Mcroatia Zdravko Logarusic kwa pamoja na wasaidizi wake Suleiman Matola na Iddi Pazi waliwafuata marefa katikati ua Uwanja kuwalalamikia walikuwa wanawapendelea wenyeji na kuwaomba kipindi cha pili wachezeshe haki.

Ramadhani Singano 'Messi' wa Simba SC akiwatoka mabeki wa Mbeya City leo



Kipindi cha pili, Simba SC ilibadilika mno na kuongeza kasi ya mashambulizi, hatimaye kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 50 mfungaji Mrundi Amisi Tambwe, aliyemalizia krosi ya Haroun Chanongo.
Baada ya Simba SC kusawazisha, kasi ya mchezo iliongezeka kwa pande zote mbili, timu zote zikishambuliana kwa zamu.
Kikosi cha Mbeya City kilikuwa; David Burhan, John Kabanda, Hamad Kibopile/Mwagane Yeya dk31, Deo Julius, Yussuph Abdallah, Anthony Matogolo, Peter Mapunda, Steven Mazanda, Paul Nonga/Francis Castor dk81, Hassan Mwasapili na Deus Kaseke.
Simba SC; Yaw Berko, William Lucian ‘Gallas’, Henry Joseph, Joseph Owino, Donald Mosoti, Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’/Awadh Juma dk66, Said Ndemla/Christopher Edward dk76 , Amisi Tambwe, Amri Kiemba na Haroun Chanongo/Zahor Pazi dk54.
Katika mechi nyingine za leo, Rhino Rangers imetoka sare ya 1-1 na Mgambo JKT Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mjini Tabora, bao la wenyeji likifungwa na Gideon Brown dakika ya 30 na wageni wakisawazisha dakika ya 52 kupitia kwa Ally Bolly.
Ashanti United imetoka sare ya bila kufungana na Kagera Sugar Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na bao pekee la Peter Michael dakika ya 49 limetosha kuwapa Prisons ushindi wa ugenini wa 1-0 dhidi ya wenyeji Mtibwa Sugar Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
JKT Oljoro imetoka sare ya bila kufungana na JKT Ruvu Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, wakati bao pekee la Said Dilunga dakika ya 85 limeipa Ruvu Shooting ushindi wa 1-0 dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

No comments:

Post a Comment