Thursday, 14 November 2013
USHIRIKINA KATIKA SOKA UPO HATA ULAYA ?
HEBU msomaji cheki jinsi wenzetu wa Ulaya wanavyofanya mambo yao ya kiufundi kistaili!
10. Paul Ince
Mtaalamu huyu wa zamani wa Man united, Liverpool na timu kadhaa nyinginezo alikuwa anahakikisha anakuwa wa mwisho kutoka katika chumba cha kubadilishia nguo katika kila mechi aliyocheza. Si hapo tu bali angesubiria hadi sekunde ya mwisho kabla mchezo kuanza ndipo angevaa jezi yake. Wadau hatujui hii ilimsaidia nini!
9. Laurent Blanc
Nani anakumbuka fainali za kombe la dunia mwaka 1998? Kama una kumbukumbu nzuri utajua kwamba beki wa zamani wa Ufaransa na kocha wa sasa wa timu hiyo hiyo laurent Blanc, alikuwa na utaratibu wa kubusu kipara cha kipa wao Fabien Barthez kabla ya kuanza kwa kila mechi. Sasa sijui alikuwa akionesha mapenzi yake kwa Barthez ama ilikuwa kwa ajili ya kupata bahati, ukweli ni kwamba ilisaidia kwani Ufaransa waliibuka mabingwa mwaka huo!
8. Steven Pienaar
Kila timu huwa na sala zao kabla ya mechi lakini mwaka huu timu ya taifa ya Sauzi Bafana Bafana ilitoa mpya pale wachezaji wote walipokuwa wakishika kichwa cha Steven Pienaar na kupeana maneno ya kutia moyo kabla ya kila mechi.
7. David James
Walinda milango huwa wanajulikana kwa kuwa watu wa ajabu. Kipa wa Uingereza David James ni mmojawapo wa watu hawa. lakini mwaka huu alizidi kipimo kwani alikuja na staili ya kujitupa na kudaka hewa kabla ya kila mechi akidai kwamba hii inamsaidia kujiweka fiti kabla mechi. Sisi tunajiuliza kwa nini adake hewa na asitumie mpira wa ukweli?
6. Johan Cruyff
Sasa hii hadi najisikia kucheka! Nguli huyu wa soka wa Uholanzi alikuwa mmojawapo wa wachezaji bora, kama si mchezaji bora kupata kutokea katika nchi ya Uholanzi. Lakini yaelekea ubora huo ulichangiwa na kitu fulani kwani jamaa huyu alikuwa ana tabia ya kumchapa bonge la kibao cha tumbo kipa wake na baadae kwenda kutema bigijii yake katika lango la timu pinzani kabla ya kila mchezo. Usiniulize maumivu aliyokuwa akipata kipa wake, si bora angembusu tu!
5. Bobby Moore
Nahodha wa timu ya Uingereza iliyokuwa mabingwa wa dunia mwaka 1966 alikuwa na katabia kamoja kakushangaza sana. Jamaa huyu alikuwa anahakikisha anakuwa wa mwisho kuvaa kaptula yake kabla ya mchezo. Na iwapo kama kuna mchezaji mwingine ataamua kubadilisha kaptula yake katikati ya mchezo, mtaalamu Bobby More atahakikisha anavua ya kwake na kuvaa tena.
4. Gary Lineker
Mmojawapo wa wafumania nyavu wakali kupata tokea katika timu ya Uingereza alikuwa akiwashangaza wengi pale alipokuwa akiepuka kabisa kufanya mazoezi ya kupiga mashuti kabla ya mechi. Alisema kwamba huwa hafanyi mazoezi ya kupiga mashuti sabau alikuwa hataki kupoteza magoli yake bure na alikuwa akiyahifadhi kwa ajili ya mechi. Hakuishia hapo tu mzee mzima kama hakupata bao katika dakika 45 za mwanzo alikuwa akihakisha anabadili jezi yake na kuvaa nyingine kuondoa nuksi.
3. Raymond Domenech
Kocha asiyeeleweka wa Ufaransa, Domenech alikuwa ana tabia ya kuchangua wachezaji kutokana na nyota zao. Kuna wakati kiungo Robert Pires aliachwa katika timu sababu alikuwa ana nyota ya Scorpio ama nge. Kajaribu vyote lakini kashindwa kusafisha nyota yake mwenyewe kwani hivi sasa anahaha kutafuta kibarua.
2. Adrian Mutu
Inasikitisha kuwa Mutu hatopata tena nafasi ya kufanya mambo yake ya kishirikina hivi karibuni sababu ya adhabu ya kisoka anayotumikia kwa ajili ya matumizi ya dawa za kulevya. Lakini enzi zake mtu huyu alikuwa akihakikisha anavaa chupi yake nje ndani katika mechi yoyote ile anayocheza. Alipoulizwa kwanini anafanya hivyo, Mutu alijibu kuwa kama hainiumizi kwanini nisifanye!
1. Shay Given
Kutakuwa kuna kitu tu nyuma ya magolikipa wa nchi ya Ireland, tukiangalia kipa wao wa zamani Pattie Booner ambaye alikuwa ana tabia ya kubeba kipande cha udongo katika mkoba wake wa glovu za kipa. Tukija kwa kipa wa sasa Shay Given ambaye huwa anahakikisha ana chupa ya maji matakatifu” nyuma ya goli lake kila wakati. Given alikuwa hachezi mechi bila chupa yake ya maji!Wabongo mpo hapo?
www.tabasamuleo.blogspot.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment