Thursday, 14 November 2013
Dawa yako Kaseja inakuja
Juma Kaseja
By LASTECK ALFRED,MWANASPOTI MASTRAIKA wawili tegemeo wa Simba, Amissi Tambwe na Betram Mwombeki, wameingia msituni kufanya jambo ambalo si zuri kwa Yanga hususani mabeki wa timu hiyo na kipa wao mpya, Juma Kaseja.
Kaseja amesajiliwa Yanga kuongeza nguvu kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika katika mechi zitakazochezwa mwakani.
Mwombeki na Tambwe walichangia kuivuruga Yanga kiuchezaji kwenye mechi ya watani wa jadi iliyomalizika kwa sare ya mabao 3-3 ambapo Simba ilifunga mara tatu kipindi cha pili kufuta yale ya Yanga ya kipindi cha kwanza.
Wachezaji hao wameanza programu zao nzito za mazoezi ambazo lengo lake ni kuwaongezea nguvu zaidi za kupiga mashuti na kupambana na mabeki imara wakiwemo wa timu ngumu kama Yanga, Azam na Coastal Union.
Mrundi Tambwe amemsisitiza Mwombeki kujiandaa kwa moto uleule akisema: “Mwombeki ana nguvu, lakini anahitaji kujiimarisha zaidi ili aweze kuwa na kazi nyepesi mbele ya mabeki wakorofi na wenye kutukamia badala ya kucheza mpira.
“Akishakuwa na nguvu ya kupambana na ubabe wao, wenyewe wataogopa na kuanzia hapo kazi itakayobaki ni kufunga magoli kama ilivyo mipango yetu ya kuanzia ligi ilipoanza, tunataka kufanya kazi kwa nguvu,” alisema.
Tambwe alisema yeye na Kaze wamepanga kuanza mazoezi Jumatatu kwenye klabu yao ya zamani ya Vital’O. Mwombeki amesema wiki mbili za mapumziko , atazitumia kukaa na familia yake tu lakini baada ya hapo ataanza mazoezi makali.
“Nina programu yangu maalum ya mazoezi pamoja na mapumziko, nataka nikirudi kwenye mzunguko wa pili nije kwa nguvu. Mimi ni profeshno (mchezaji wa kulipwa) nahitaji kufanya kazi sana na naamini kwamba nikimaliza mazoezi yangu nitakuwa fiti, Mungu akijali nitakuja vizuri sana kwenye mzunguko wa pili,” alisema Mwombeki.
Endapo wachezaji hao watakuja fiti huenda wakaitetemesha Yanga iliyopo kileleni kwa pointi 28. Azam ina pointi 27 sawa na Mbeya City, Simba ina pointi 24 ikishikilia nafasi ya nne. Simba itacheza mechi nane za mzunguko wa pili jijini Dar es Salaam huku nyingine tano ikicheza mkoani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment