Na Amran Muhina, Dar es Salaam
RAIS wa zamani wa klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam, Tarimba Abbas amesema kwamba ana dhamira ya kurudi kuiongoza klabu hiyo, katika uchaguzi ujao uliopangwa kufanyika Juni 15, mwaka huu.
Tarimba ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, kwa sasa bado mapema mno kuzungumzia jambo hilo ingawa kama mwana-Yanga ana haki yake kikatiba.
“Ni mapema mno kusema nitagombea, maana uchaguzi ni mpaka Juni ni kipindi kirefu sana, lakini kama mwana-Yanga dhamira ninayo ingawa inaweza isiwe sasa, ila ninachoweza kusema ni mapema mno kuzungumzia jambo hilo,” alisema Tarimba.
Tarimba kulia akizungumzia pembeni ya Mkurugenzi wa Masoko wa Vodacom, Kevin Twissa
Tarimba ambaye kwa sasa ni kada wa CCM, Diwani wa Kata ya na Mkurugenzi wa Tume ya Michezo ya Kubahatisha ni kati ya watu ambao wana Yanga SC wanawataka sana waingie kuongoza klabu hiyo pamoja na Davis Mosha.
Angu Shadrack na wanachama wenzake vijana wa Kariakoo wanajipanga kumfuata Davis Mosha kumshawishi achukue fomu za kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti, wakati Tarimba Abbas wanataka awania Uenyekiti wa klabu hiyo.
“Tunajipanga kuwafuata Mosha na Tarimba kuwaomba wagombee, hawa viongozi wetu wa sasa wametuangusha sana, tunataka watu ambao hatutawajaribu, tunajua ni watu wa kazi na wana mapenzi na Yanga,”alisema Angu.
Gazeti la Spoti Leo la leo nalo limewanukuu wanachama wa Yanga wakisema wanaamini Tarimba anastahili kuvaa viatu vya Manji kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha wakati akiwa Rais wa Yanga mwanzoni mwa miaka ya 2000.
“Tumeshakaa mara kadhaa wana-Yanga kujadili nani anafaa kuongoza baada ya Manji kumaliza muda wake, lakini wengi mawazo yetu yameangukia kwa Tarimba. Tunaamini ni kiongozi mzuri na anaweza kuipeleka Yanga pazuri,” alisema Juma Mohammed ‘Kamanda’ aliyejitambulisha anatoka Yanga Bomba.
Naye mwanachama mwingine wa Yanga, Suleiman Mussa, alisema wameanza mikakati ya kuangalia nani atafaa kuiongoza Yanga na wanajipanga kwenda kumuona Tarimba ili kumshawishi wakati ukifika ajitose kwenye uchaguzi huo.Uongozi wa sasa wa Manji uliingia madarakani Julai 15 mwaka juzi katika uchaguzi uliofanyika kuziba nafasi za viongozi kadhaa waliojiuzulu kutokana na sababu mbalimbali katika uongozi uliochaguliwa Julai 18 mwaka 2010 kwenye viwanja vya Maonesho ya Sabasaba, Dar es Salaam, ambapo Wakili Lloyd Nchunga alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Yanga akichukua nafasi ya Imani Madega ambaye hakugombea.
Wengine waliochaguliwa siku hiyo ni Davis Mosha ambaye aliibuka Makamu Mwenyekiti, wakati wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Ally Mayai, Mzee Yusufu, Sarah Ramadhani, Tito Osoro, Mohamed Bhinda, Charles Mngodo, Salum Rupia na Theonest Rutashoborwa.
Hata hivyo, wajumbe kadhaa walijiuzulu akiwemo Nchunga, Mosha, Mzee Yusuph na Mayai, huku Rutashoborwa akifariki dunia, hali iliyoifanya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuitaka Kamati ya Uchaguzi ya Yanga iitishe uchaguzi.
Katika uchaguzi huo mdogo wa mwaka 2012 kujaza nafasi mbalimbali zilizokuwa wazi ulishuhudia Manji akiibuka Mwenyekiti, huku Clement Sanga akiwa Makamu Mwenyekiti, ambapo wajumbe wengine waliochaguliwa siku hiyo walikuwa ni, Abdallah Bin Kleb, Moses Katabaro, Aaron Nyanda na George Manyama.
Uongozi wa sasa wa Manji ‘umefeli’ na kupoteza kabisa imani mbele ya mashabiki na wanachama wa timu hiyo, hali ambayo imeyafanya makundi ya wanachama yaanze mchakato wa kusaka viongozi bora.
No comments:
Post a Comment